Sunday, 13 March 2016

WAFUKIWA WAKIIBA MADINI


 
WACHIMBAJI wadogo watatu wanasadikiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi, wakati wakiwa kwenye harakati za kuiba madini ya tanzanite katika mgodi wa Tanzanite One, Mirerani.
Taarifa ya kufukiwa kwa wachimbaji hao maarufu kama Wanaapolo, ilitolewa jana na mchimbaji mwenzao, Gidish Benedict (32), aliyekuwepo eneo la tukio na kunusurika wakati wenzake wakifukiwa.
Kwa mujibu wa Benedict aliyezungumza na waandishi wa habari mjini hapa, hajui kama wenzake watakuwa hai, kwani sehemu waliyokuwepo haikuwa na hewa hivyo kuna uwezekano wa wenzake watatu kufa wakiwa huko chini.
Aliwataja wenzake hao waliofukiwa kuwa ni Saidi Mgosi, mkazi wa Boma mkoani Kilimanjaro na wengine aliowataja kwa jina moja kuwa ni Dominic, mkazi wa Zaire Mirerani kwa jina la utani anaitwa Bwashee na Khalid, ambaye hafahamu anakotoka.
“Sijui kama wenzangu wapo hai au la maana nilimwambia mbona nguzo imebana sana, wakasema toka wewe si mzoefu wacha sisi wazoefu tufanye kazi. “Nilijibanza pembeni ya mwamba na kuwapisha watengeneze njia ili tutoke, lakini wakati wakigonga nguzo, udongo ulimwagika kwa kasi mimi nikarudi kwenye upenyo nikafanikiwa kupona, lakini sijui wenzangu kama wapo hai watakuwa wamefukiwa na kifusi,” alisema.
Amekiri kuwa walizama ndani ya mgodi huo Jumatatu ya wiki hii saa 7 usiku kwa njia za panya maarufu ‘bomu’, lakini wenzake wamefukiwa na kifusi na haijulikani kama wako salama.
*Tanzanite One
Akizungumzia jana Mirerani, Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Sky Associates, inayomiliki mgodi huo wa Tanzanite One, Apolinary Modest alisema Wanaapolo hao waliingia katika mgodi huo uliofungwa Jumatatu wiki hii na kuanza kuchimba madini.
Kwa mujibu wa Modest, baada ya kumaliza kazi hiyo walianza safari ya kurudi juu, lakini walishindwa kufika juu siku ya Ijumaa, baada ya kugonga nguzo ambayo ilitoa udongo mwingine uliosababisha njia hiyo ya panya kuziba.
“Hivi sasa tupo na wataalamu wetu wa uokoaji kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kuwaokoa Wanaapolo hawa ambao hatujui kama wapo hai au la. “Bado kama mita mbili au tatu kufika eneo la tukio chini ya ardhi ili kuona kama wapo hai au wamekufa au wamepita njia nyingine za panya na kukimbia,” alisema Modest.
Alisema njia za panya zipo nyingi na kampuni imejitahidi kuziba, lazini zinazibuliwa na Wanaapolo ili kuingia ndani ya mgodi uliofungwa au unaoendelea kuchimbwa madini hayo kwa nia ya kuiba madini.
Modest alisema machimbo yapo mengi zaidi ya 100 ambayo yamezibwa, lakini Wanaapolo hao wamekuwa wakizibua kwa njia zao na kuingia eneo la Tanzanite One, ili kuiba madini hayo na mchimbaji huyo aliye hai, anashirikiana na waokoaji kuonesha njia walizopita ili wenzake waokolewe.
Wanaowapeleka Shuhuda huyo, Benedict aliendelea kusema kazi hiyo ya kwenda kuiba madini, hufadhiliwa na wafanyabishara wakubwa wa madini ambao hutoa mamilioni ya fedha kwa wachimbaji hao ili wafanikishe wizi huo.
Alisema wao hawana nia mbaya, bali husukumwa na wafanyabiashara hao ambao hutenga mamilioni ya fedha kwa kazi hiyo. ‘’Sisi tunanunuliwa zana zote za uchimbaji na tunatumwa kwenda kuiba madini Tanzanite One na huko chini ni usalama wako ndio unakulinda na ukipata madini, unampelekea kwa aliyekufadhili ambaye ni mafanyabiashara mkubwa wa tanzanite.
“Naomba mnisamehe maana msukumo ndio unatufanya tufanye kazi hii ya bomu na njaa pia inachangia,’’ alisema. Kamanda wa Polisi wilayani Simanjiro, Francis Massawe amethibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa bado wanaendelea na uokozi. Imeandikwa na Veronica Mheta na John Mhala, Arusha.

No comments:

Post a Comment