Aidha Makalla aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kumpa taarifa za maandishi kuhusu mahitaji ya madawati, yaliyopo kwa sasa na upungufu uliopo. Akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Charles Mlingwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Moses Jonas, Makalla alisema viongozi wa wilaya hizo wanafanya upotoshaji kuficha upungufu uliopo, jambo alilosema litawagharimu.
“DC umepata ujumbe wangu kuhusu madawati? Fanyia kazi haraka, nimetaka takwimu za madawati zaidi ya mara tano mnanipiga chenga, sasa natoa saa saba mnipe maandishi kama hakuna upungufu mnieleze...ili mkinidanganya mtakuwa mmejifukuzisha kazi,” alisema.
Aidha Mkuu wa Mkoa alielezea kushangazwa na taarifa za Mkurugenzi wa Wilaya ya Hai, Said Mderu kwamba hawana upungufu wa madawati licha ya mkuu wa wilaya hiyo, Anthony Mtaka kueleza jinsi ya kukabili upungufu uliopo.
“Wakati naongea na Mtaka amenieleza wanapambana kupata madawati huku mkurugenzi ananieleza hawana upungufu kwa shule za msingi na sekondari jambo ambalo linatia shaka,” alisema.
Alisema taarifa za uongo zitawagharimu viongozi hao wakati viongozi wa kitaifa, hususan mawaziri, Waziri Mkuu au Rais watakapowatembelea. “Hizi taarifa zenu za kupika zitawagharimu pale atakapokuja waziri kisha azungumze na wananchi ambao wataeleza hali halisi ikiwamo baadhi ya wanafunzi kukalia ndoo darasani... semeni kweli maana upungufu huo ni matokeo chanya ya elimu bure,” alisema.
Januari mwaka huu, Makalla alitaja wilaya ambazo zina upungufu wa madawati na idadi yake kwenye mabano ni wilaya ya Mwanga (867), Same( 592) na Siha (282) .
No comments:
Post a Comment