Kutokana na ukweli huo, baraza hilo limewaonya wamiliki wa viwanda, nyumba za ibada, waendesha bodaboda na wamiliki wa baa au kumbi za starehe, kuhakikisha wanafuata Sheria ya Utunzaji wa Mazingira kwa kuepuka kupiga makelele na mitetemo katika maeneo ya makazi.
Tayari Baraza hilo, limeshawachukulia hatua wamiliki wa nyumba za ibada na kumbi za starehe ikiwemo klabu ya TCC Chang’ombe kwa kukiuka sheria hiyo na kupiga kelele na mitetemo katika maeneo ya makazi ya watu na kuitoza faini ya Sh milioni 15.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo, Bonaventura Baya, alisema uharibifu huo wa mazingira, unazidi kukithiri kutokana na ujenzi holela wa makazi, matumizi holela ya rasilimali ardhi na kelele kutokana na shughuli za binadamu.
Alisema katika miji hiyo, kumekuwepo na uanzishwaji wa viwanda sehemu zisizo rasmi ambazo ni karibu na makazi ya watu pamoja na viwanda vingi kukosa miundombinu ya majitaka hivyo kutitirisha hovyo majitaka na kuchafua mazingira.
“Ukweli hali ya miji hii ni mbaya katika mji wa Dar es Salaam ambao ni wa nne kwa ujenzi wa kasi duniani kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia wa mwaka 2015, kasi ya ujenzi wa majengo ya kisasa ni kubwa. Ujenzi huu umekuwa ukihitaji mchanga, kokoto, saruji, nondo na viwanja,” alisema.
Alisema kutokana na mahitaji ya vifaa hivyo kuwa makubwa, kumekuwa na lindi kubwa la uvamizi wa maeneo ya wazi hasa mabondeni, pembezoni mwa barabara, kwenye mito na uchimbaji holela wa mchanga na kokoto hali inayochangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Kuhusu kelele katika maeneo ya makazi, Baya alisema tatizo hilo linatambuliwa kuwa kero kisheria na tayari kupitia aliyekuwa Waziri mwenye dhamana ya mazingira Dk Binilith Mahenge, alizindua kanuni za usimamizi wa mazingira za viwango vya kelele na mitetemo za mwaka jana.
Alisema kupitia kanuni hizo baraza hilo, limefanikiwa kutoa onyo, kuweka zuio na kutoza faini kwa waliosababisha kelele hizo ambao ni kampuni ya CRJ iliyotozwa faini ya Sh milioni 50, ukumbi wa starehe wa Matei Lounge uliopo Dodoma ulitozwa faini Sh milioni tano na TCC klabu faini milioni 15. Aidha baraza hilo limetoa onyo kwa nyumba za ibada ambazo ni Kanisa la Show Army lililopo Sinza na Kanisa la Mlima wa Moto.
Baya pia alisema baraza hilo limepokea tangu mwaka huu, uanze malalamiko zaidi ya 100 yanayohusu uharibifu wa mazingira ikiwemo, malalamiko dhidi ya kelele zinazosababishwa na waendesha bodaboda. “Tumepanga kukutana na vyama vya waendesha bodaboda kuzungumzia namna ya kulipatia ufumbuzi lalamiko hili.”
Baraza hilo, limetoa changamoto kwa Serikali kuanza kuchukua hatua za haraka kuokoa miji hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inaboresha huduma za mipango miji na kuweka mikakati chanya ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
Alizitaka halmashauri za miji kusimamia Sheria zilizopo ikiwemo za madini, mazingira na sheria ndogo za mipango miji kwa ajili ya kudhibiti waharibifu wa mazingira wakiwemo wachimbaji hovyo wa mchanga na kokoto na ujenzi holela wa makazi.
No comments:
Post a Comment