Sunday, 6 March 2016

Mawaziri watatu kutatua mipaka Simiyu, Serengeti

 

 

 

 


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema atawatuma mawaziri watatu waende mkoa wa Simiyu ili wakae na uongozi wa kila wilaya pamoja na wananchi ili kubaini tatizo la mipaka baina ya wilaya hizo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa vijiji vya Mwakaluba na Mwandoya akiwa kwenye siku ya tano ya ziara yake mkoani Simiyu.
“Tangu niingie hapa mkoani malalamiko ya mipaka nimeyapokea kila mahali nilikopita. Nimeamua kuwatuma mawaziri watatu ambao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawene, waje mkoa huu kutatua matatizo yenu,” alisema.
Aliongeza kuwa, “nitawatuma waje na wapite kila wilaya, wakae na kuzungumza na wakulima na wafugaji ili kubaini ni chanzo cha tatizo la migogoro hii kwenye mipaka ya vijiji na hifadhi ya Serengeti. Pia Waziri wa TAMISEMI itabidi atoe ufafanuzi kuhusu agizo lao la kutofanya shughuli yoyote mita 60 kutoka kwenye mto Simiyu ili wananchi waelewe."
Mapema Mbunge wa Kisesa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais(Mazingira), Luhaga Mpina alimweleza Waziri Mkuu mbele ya wananchi hao kwamba limetolewa zuio linalowataka wakazi wa mkoa huo wasifanye shughuli zozote umbali wa mita 60 kutoka kwenye kingo za mto huo.
Ili kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi hapa nchini, Waziri Mkuu alisema serikali ina mpango wa kuunda mabaraza ya ardhi 100 kwa nchi nzima ambayo yatakuwa na jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati.
Akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Erasto Sima alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Julai mosi, 1987 ina ukubwa wa kilometa za mraba 8,835 ambapo asilimia 49 (sawa na kilometa za mraba 4,329) ya eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za wanyamapori.
Alilitaja eneo hilo kuwa ni pori la akiba la Maswa, sehemu ya hifadhi ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na pori la hifadhi ya usimamizi wa wanyama (WMA) la Makao na kwamba asilimia 51 iliyobakia indiyo inayotumiwa kwa makazi ya watu, kilimo na malisho ya mifugo.

No comments:

Post a Comment