Wednesday, 30 March 2016

Magufuli atua kwa kishindo Mwanza

Rais Dk John Magufuli akitokea katika mgahawa wa Victoria alikopata chakula cha mchana jijini Mwanza.


RAIS John Magufuli ametua kwa kishindo mkoani Mwanza kwa mara ya kwanza akiwa njiani kwenda nyumbani kwao Chato mkoani Geita tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwishoni mwa mwaka jana.
Ikiwa ni mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kuwasili mkoani Mwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Rais, ndege yake ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 5.11 asubuhi na yeye alikanyaga ardhi ya Mwanza saa 5.19 akiwa amefuatana na mkewe Janeth Magufuli akiwa njiani kwenda Chato kwa mapumziko.
Mara baada ya kutua, aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kumaliza na kutatua kero ya muda mrefu ya barabara ya Airport- Kayenze –Igombe (kilometa 24) iliyokuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa Igombe kwa kuagiza barabara hiyo ifunguliwe mara moja.
Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kuhakikisha kuwa wanafungua vizuizi vyote vilivyowekwa kwenye barabara hiyo mara moja ili kuwawezesha wananchi wa Igombe na Kayenze kuitumia barabara hiyo kuja mjini kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
“Msimamo wangu bado haujabadilika, hakuna kuifunga barabara ya Kayenze – Igombe kwa sasa ili wananchi wa Kayenze wasihangaike kuja mjini, nakueleza Mkuu wa mkoa, wewe ndiye Mkuu wa mkoa nisije nikasike barabara hiyo imefungwa tena,” alisema huku akishangiliwa na hadhara iliyokuwa uwanjani.
Kwa upande wake, Mongela alimueleza Rais kuwa baada ya yeye kuondoka kwenda Chato, atakwenda moja kwa moja kuondoa vizuizi vyote vilivyowekwa katika barabara hiyo. “Nikuhakikishie baada ya wewe kuondoka hapa, nitakwenda moja kwa moja kuondoa vizuizi vilivyo kwenye barabara hiyo ili ianze kutumiwa na wananchi,” alisema Mongella.
Kufunguliwa kwa barabara hiyo, kutawaondolea adha wananchi waliokuwa wanalazimika kutembea mwendo mrefu wa kilometa 40 wakizunguka kupitia Buswelu kwenda Mwanza Mjini kutafuta mahitaji yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mwanza, Leonard Kadashi alisema barabara ilifungwa na uongozi wa uwanja wa ndege ili kupisha ukarabati uliokuwa ukiendelea uwanjani hapo.
Akiwa uwanjani hapo, Dk Magufuli alipokewa na Mongella na viongozi wengine wa mkoa akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Dk Anthony Diallo, na baadaye aliombewa dua na Imamu wa Msikiti wa Ibadh Shehe Nuhu Othmani na sala na Mchungaji Alex Rwakisumbwa wa Tabernacle Gospel Church International la jijini Mwanza.
Alifurahishwa na Kwaya ya Vijana ya AIC Makongoro iliyokuwa ikiimba wimbo wa amani ambayo alijumuika nayo kuimba wimbo huo huku akicheza pamoja na wanakwaya. Aliwashangaza watu waliojitokeza uwanjani hapo badala ya kuingilia eneo la VIP alipitia mlango mwingine ulio karibu na VIP na kusalimiana na wasafiri na wafanyakazi wa uwanja huo kabla ya kurudi tena VIP.
“Jamani hamjambo? Niliona nisipite bila ya kuwashika mikono,” alisema Rais huku akiwapungua mkono. Aidha, Rais na mkewe waliwashangaza wananchi baada ya kwenda kula chakula na wananchi kwenye mgahawa maarufu wa Airport ambako alitoa ofa maalumu ya kuwanunulia soda wananchi waliokuwa nje ya uwanja.
“Jamani karibuni tule chakula pamoja, wananchi wote waliopo hapa karibuni tunywe soda pamoja nitalipa bili,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wananchi waliokuwa nje ya eneo la uwanja wa ndege.
Rais aliwapongeza wakazi wa Mkoa wa Mwanza kwa kumuonesha upendo mkubwa kwa kumchagua kwa kura nyingi za kishindo kuliko mikoa mingine, huku akiwaahidi hatawangusha na kwamba bado anakumbuka ahadi aliyowaahidi ya kuwanunulia meli itakayofanya safari zake kutoka Mwanza hadi Bukoba.
“Nawashukuru sana kwa kunichagua kwa kura nyingi sana, wakati mwingine huwa najiuliza niwalipe nini wana Mwanza, lakini nawaahidi sitawaangusha,” alisema Dk Magufuli na kuahidi kutenga fedha katika bajeti ya mwaka ujao kumalizia ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Aliwashukuru viongozi wa madhehebu ya dini nchini kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakitekeleza utume wa kazi zao kwa kumuombea yeye na Serikali yake na kuwataka wasichoke kufanya hivyo kwa kuwa Tanzania ni ya wote

No comments:

Post a Comment