Tuesday, 8 March 2016

Marufuku kupandisha bei ya sukari


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles Mwijage

BODI ya Sukari Tanzania imewataka wafanyabiashara kutopandisha bei ya sukari huku ikiwasisitiza kuheshimu bei elekezi iliyopo. Aidha, imesema inazo taarifa kuhusu wafanyabiashara wakubwa, ambao kwa sababu wanazozijua, wameamua kuficha sukari hatimaye wapandishe bei, kitendo ambacho itachukua hatua dhidi yao.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Henry Semwaza alisema sukari inatakiwa kuuzwa Sh 2,000 katika jiji la Dar es Salaam na mikoa jirani. Kwa upande wa maeneo ya pembezoni, itauzwa kwa bei isiyozidi Sh 2,200 kwa kilo kutokana na gharama za usafirishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Semwaza alisema upatikanaji wa sukari nchini ni wa kuridhisha na ipo akiba ya kutosheleza nchi nzima. Alisema pamoja na baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji wa sukari kutokana na msimu kuisha, hali ya sukari nchini ni nzuri na ipo akiba zaidi ya tani 62,000. “

Upatikanaji wa sukari nchini ni wa kuridhisha na hakuna haja ya kuwa na hofu ya upungufu wa bidhaa hiyo, kwani ipo katika mikoa yote nchini,” alisema. Aliendelea kusema, “ Kuna wafanyabiashara wakubwa ambao kwa sababu wanazozijua wenyewe wameamua kuficha sukari ili kupandisha bei.
Watu hao watakapobainika watachukuliwa hatua za kisheria na wananchi wanatakiwa kuwafichua watu hawa.” Aliwataka wasambazaji wakubwa wa sukari hususan kampuni ya Alneen Enterprise ya jijini Dar es Salaam, ambayo imethibitisha kuwa na sukari tani 8,600 kuitoa na kuiuza.

“Nawaagiza kampuni ya sukari ya TPC na Kilombero watoe sukari kwenye maghala yao na kuiuza, agizo hili linakwenda kwa kampuni ya Alneen watoe sukari mara moja ili kuondoa kile kinachoonekana kama upungufu usio halisi wa bidhaa hiyo hapa nchini,” alisema.

Aidha, Semwaza alisema Bodi ya Sukari Tanzania kwa kushirikiana na Kamati Ufundi ya Uagizaji wa Sukari nchini na Sekretarieti za mikoa, itaendelea kufuatilia kwa karibu kiasi cha sukari kilichopo nchini na mwenendo wa bei na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wafanyabiashara watakaoharibu mwenendo wa soko.

Wakati huo huo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles Mwijage alisisitiza kuwa hakuna uhaba wa sukari nchini na kuwataka wafanyabiashara walio na leseni za kuingiza na kuuza bidhaa hiyo, kutoificha.
Mwijage alitaka watu wenye taarifa juu ya mfanyabiashara aliyefungia sukari katika ghala lake ampelekee, afunge ghala husika mara moja. “Hakuna upungufu wa sukari nchini, na tunayo akiba ya kutosha ya sukari na kama kuna mtu mwenye taarifa juu ya mfanyabiashara aliyeficha na kuzuia kuuza sukari katika ghala lake nitaenda mwenyewe kulifunga,” alisema Mwijage.
Alisema serikali inajikita zaidi katika uanzishaji wa viwanda vya sukari na kuongeza ajira na si katika kuagiza sukari kutoka nje. Kwa mujibu wa waziri, ofisi yake inafanya mazungumzo na mwekezaji anayetaka kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha sukari Kigoma.
Alisema wakati wowote mwekezaji atawasili nchini kukamilisha taratibu. “Kuna kampuni nyingine zimeonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya sukari nchini, na kwa sasa tunaendelea na mazungumzo na mwekezaji ambaye anataka kuja kuwekeza kwa kujenga kiwanda kikubwa cha sukari mkoani Kigoma,” alisema Mwijage

No comments:

Post a Comment