Amesema kutokana na rasilimali zilizopo, Tanzania inaweza kukidhi bajeti yake kwa asilimia 80 bila kutegemea msaada kutoka nje na kwamba suala la kukabiliana na ufisadi na ukwepaji kodi ni endelevu.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo juzi mjini Lamadi wakati akihutubia maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku sita mkoani Simiyu. “Tanzania inaweza kujitegemea kwa asilimia 80 kwa mapato yake kutokana na rasilimali na vyanzo vyake vya ndani.
Hili linawezekana. Ndio maana tumeamua kubanana,” alieleza Waziri Mkuu. Alisema ndio maana wameamua kupambana na ufisadi na ukwepaji kodi kwa nia ya kuhakikisha wanapata fedha za kuwatumikia Watanzania kwa fedha za ndani kupitia mapato yake.
Alisema hata uamuzi wa kupitisha fedha zote katika Mfuko Mkuu wa Serikali ulikuwa na nia ya kutambua mapato yake yote ili fedha hizo zikasaidie kuleta maendeleo ikiwamo kuisimamia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kubana mianya yote ya ukwepaji kodi.
Alisema hali hiyo imesaidia kwani mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 1.3 Desemba mwaka jana, Sh bilioni 1.5 Januari mwaka huu na mwezi uliopita, alisema ana hakika zitavuka zaidi.
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali ndio maana inagharimia mambo yake mengi likiwamo suala la elimu bure, na kwamba licha ya kuwapo kwa changamoto mbalimbali, watahakikisha Watanzania wanapata huduma mbalimbali zilizoboreshwa.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2015/16, Juni mwaka jana, alisema jitihada za kuongeza mapato zimelenga kuisaidia Serikali kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali kwa fedha za wahisani.
Alisema kiwango cha utegemezi kimepungua kutoka asilimia 24 mwaka 2004/05 hadi asilimia 17 mwaka 2010/11. Alisema pia kwamba utegemezi huo umekuwa ukipungua mwaka hadi mwaka. Mwaka 2015/16 ilitarajiwa upungue kwa asilimia 6.4.
Kuhusu suala la mipaka kati ya hifadhi na vijiji, Waziri Mkuu alisema amekwishaagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia suala hilo na kuhakikisha wanaliangalia limalizike kwa busara.
Lakini ameagiza wananchi hasa katika wilaya za Busega na Bariadi kutoingia tena katika hifadhi ambako inadaiwa wanapokonywa ng’ombe wao na askari wa Wanyamapori kwa kutozwa Sh milioni tano hadi 10.
No comments:
Post a Comment