Uamuzi huo umechukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, kutokana na vifo vya watoto wanne waliozaliwa pacha kutoka kwa wanawake wawili tofauti. Pia katika kadhia hiyo, mama mmoja ambaye watoto wake walifariki, naye alifariki. Akinamama hao wametajwa kuwa ni Suzana John ambaye alijifungulia watoto mapacha kwenye beseni katika Hospitali ya Butimba.
Watoto hao walifariki dunia kwa kukosa huduma muhimu za afya. Mwingine ni Pendo Masanja ambaye alijifungua mapacha waliokufa na yeye kupoteza maisha kutokana na upungufu wa damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure; saa moja na robo baada ya watoto wake kufariki.
Mkuu wa Mkoa alisema uamuzi wa kuwasimamisha kazi watumishi hao wa afya umefanyika baada ya kugundua kuwa kulikuwepo uzembe mkubwa wa kitaaluma pamoja na lugha chafu ambazo zilitumiwa wakati wa kuwahudumia wajawazito hao wawili. Akizungumza na madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Sekou Toure, Mulongo alisema matukio hayo yote yameleta taswira mbaya kwa Mkoa wa Mwanza kutokana na ukweli kuwa shughuli zinazofanywa na taasisi hizo zina lengo la kuokoa maisha ya watu.
Alimuagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ndalo Kulwijira kuwasimamisha kazi madaktari na wauguzi wote waliohusika katika kusababisha vifo hivyo kwenye hospitali hizo mbili tofauti. “Hospitali ya Sekou Toure ndiyo inabeba taswira ya huduma za afya kwa mkoa wetu. Kwa heshima ya hospitali hii, madaktari waliohusika kusababisha vifo katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana (Butimba) na hapa Sekou Toure tumewasimamisha kazi kupisha uchunguzi.
Hatuwezi kuwa na chombo ambacho watumishi wake hawawajibiki katika kuwahudumia watu,” alisema. Waliosimamishwa Butimba Waliosimamishwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana iliyoko Butimba kwa kuhusishwa na mjamzito aliyejifungulia katika beseni ni Dk Nathan Mbagaya, wauguzi Furaha Kingunge na Edina Mwasiga.
Mwingine ni dereva wa gari la wagonjwa, Gharib Hamad aliyedaiwa kutumia muda mwingi kufanya malumbano badala ya kumwahisha, Pendo Masanja katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure ambako alikuwa amepewa barua ya rufaa kwenda. Waliosimamishwa Sekou Toure Aliwataja waliosimamishwa kwa upande wa Hospitali ya Sekou Toure kuwa ni Muuguzi Kiongozi wa zamu siku ya tukio, Happiness Sospeter, muuguzi Angel Chacha, aliyempokea Pendo.
Wengine ni muuguzi Anna Malole na Lucy Kisura ambao walitumwa kwa nyakati tofauti kufuatilia dawa maabara ili Pendo atundikiwe dripu ya damu. Madaktari waliosimamishwa ni Dk Still Mbaga aliyekuwa mganga wa zamu, Dk Jamal Namkarara na mtaalamu wa maabara (kutoa damu) katika Hospitali ya Sekou Toure, Godfrey Silvester ambaye amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi na kuisaidia Serikali kupeleleza tukio hilo.
“Hawa wote wanasimama kazi kuanzia leo (jana) kupisha uchunguzi, lazima kama Serikali tulinde credibility (hadhi) ya hospitali yetu ya mkoa, lengo letu hasa likiwa ni kutenda haki kwa matukio yote mawili,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa. “Hawa tunawasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi, kwa kuwa malumbano yao yalisababisha kuchelewa kumpeleka Pendo Masanja katika hospitali ya mkoa, wakijua kuwa aliandikiwa barua ya rufaa.
Watasimamishwa kazi mpaka itakapothibitika baadaye”, alisema Mulongo. Alisisitiza: “Tunataka kuona haki ya marehemu Pendo Masanja na wataalamu waliomsaidia kuokoa maisha yake inapatikana. Tutaangalia ni daktari au muuguzi gani alitenda haki na tukiliacha jambo hili jinsi lilivyo litaleta manung’uniko makubwa, hivyo kama serikali tumechukua hatua.”
Aliwataka watumishi, wauguzi na madaktari wa Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure kuwa makini katika utendaji kazi wao kwa kutumia viapo vyao kuhudumia wagonjwa. Tume yaundwa Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa ameunda tume kuchunguza matukio hayo. Tume hiyo inaongozwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Richard Rumanyika na imetakiwa kukamilisha uchunguzi wake kwa siku tano.
No comments:
Post a Comment