Pia amesema atapangua walimu waliorundikana kwenye shule moja ili kuwe na uwiano sawa kwa nia ya kutatua tatizo la uhaba mkubwa wa walimu kwenye baadhi ya shule. Alisema hayo jana mjini hapa, wakati akifunga mkutano wa maofisa elimu wa mikoa na wilaya nchi nzima.
“Tutaanza na shule ambazo hali ni mbaya, baadhi ya shule zina miaka hata mitatu bila kupata walimu wapya licha ya kuwa walimu wamekuwa wakipangwa lakini hawaendi huko. “Kwenye shule moja utakuta somo moja lina walimu sita lakini shule nyingine hakuna hata mwalimu mmoja wa somo hilo hilo, hatutakubali,” alisema.
Alisema kuna mpango wa kupangua walimu ili waende maeneo yenye upungufu mkubwa ni moja ya njia ya kuboresha upatikanaji wa elimu bora. Kuhusu Sh bilioni 63 za ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo zilizoliwa, alisema mwaka jana fedha zilitolewa kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, lakini katika baadhi ya ofisi za elimu walikopewa fedha hizo, zililiwa.
“Mliokula fedha mrudishe, hatuwezi kuzuia watu wenye ubinafsi waendelee kuharibu elimu nchini. “Kuna watu darasa moja la shule ya msingi limekarabatiwa kwa Sh milioni 60, matundu ya vyoo hakuna, kila mmoja tutamsimamisha atoe maelezo kama una busara urudi na ukajitathimini,” alisema.
Alisema Jumatatu atapeleka barua kwa wakuu wa mikoa na wilaya, ili wasimamie fedha zote zilizopelekwa kwenye shule ili zifanye kazi iliyokusudiwa. “Ndugu zangu cha mtu sumu kitakutokea puani, mkarudishe fedha kama kuna mtu ametafuna, kama una kiwanja bora ukauze ili hiyo fedha ikafanye kazi iliyokusudiwa.
“Leo tunaongea ni marafiki lakini usipozingatia hili, si mnajua fedha zilizokuja Novemba tulipeleka mikoa yote muwe waangalifu sana,” alisema. Aliwataka maofisa elimu kuwa kiungo muhimu kati ya walimu, wazazi na jamii inayozunguka kwani elimu bora haiwezi kutolewa kama wazazi na jamii hawatoi ushirikiano.
“Usimamizi ni pamoja na kuangalia kunakuwa na mazingira rafiki katika utoaji wa elimu,” alisema. Pia alisema amekuwa akishangazwa na kitendo cha maofisa hao kujilipa fedha nyingi kwa ajili ya mafunzo, huku watoto wananyeshewa mvua.
“Mtu bila aibu anaweka Sh milioni nne kwa mafunzo ya mtu moja, tuwe na aibu kidogo kama hamna mtafute mahali mkaazime. “Ni kitu gani kinafundishwa kwa siku nne kwa Sh milioni 4 mtu mmoja milioni moja, sasa safari zote zinafutwa fedha zinakwenda kujenga madarasa,” alisema.
Alisema kuna hela kidogo zitapelekwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na kipaumbele ni kuwatoa watoto nje wakae ndani kwenye madawati. “Kila mtu anayeitakia mema Sera ya Elimu ni kuweka kipaumbele, tumekuwa wabinafsi sana, mtu anafikiria atapata nini kwanza... huu ni wakati wa kutumikia wananchi ili elimu yetu isimame na ipate heshima,” alisema.
Alisema maeneo yote ya mafunzo ya kujenga uwezo, yatatakiwa yasimame ili fedha ziweze kwenda kujenga na kuimarisha miundombinu. Alisema mwaka huu kwenye elimu lazima kufunga mkanda ili kilio cha kuwatoa watoto katika mazingira ambayo hayapendezi kimalizwe. Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Elimu wa Mikoa na Wilaya (REDEOA), Juma Kaponda alipendekeza mitihani ya kidato cha nne na maarifa irudi mwezi Oktoba.
No comments:
Post a Comment