Wekundu hao wa Msimbazi huenda wakapanda kileleni tena iwapo watafanikiwa kuwafunga Ndanda Fc katika mchezo huo kwa kuwa watafikisha pointi 51 na kuishusha Yanga yenye pointi 50.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Simba ilikaa kileleni kwa siku mbili kabla ya Yanga juzi kupanda na kumpiku kufuatia ushindi wake wa mabao 5-0 dhidi ya African Sports ya Tanga. Simba, Yanga na Azam FC zinatofautiana kwa pointi chache kiasi kwamba mmoja akishinda, mwingine anashuka.
Simba ina uwezekano wa kushinda mchezo wa Ndanda, kwani katika mchezo wake wa raundi ya kwanza ilishinda bao 1-0 ugenini mjini Mtwara. Hali itakuwa mbaya kwa Ndanda kama itakubali kichapo kwa mara nyingine kwani licha ya kuwa katika nafasi ya nane, ina pointi 24 ambazo hazitoshi kuihakikishia kubaki salama kwenye msimamo wa ligi kwa kuwa timu zilizoko chini yake zinaweza kupanda kutokana na kutofautiana pointi chache.
Kwa upande wa Mbeya City, huenda ikafanya vizuri leo baada ya kuonesha kiwango bora chenye mabadiliko katika mchezo dhidi ya Simba wiki iliyopita. Licha ya kufungwa mchezo huo, walicheza vizuri isipokuwa inayumbushwa na ubutu wa safu yake ya ushambuliaji.
Pengine kwa vile inacheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wanaweza kutumia faida hiyo katika kufanya vizuri na kufuta machungu ya kufungwa na timu hiyo ya Shinyanga bao 1-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza.
No comments:
Post a Comment