Tuesday, 8 March 2016

Yanga yanyemelea nafasi ya kwanza ligi kuu ya Tanzania Bara



YANGA leo itakuwa mwenyeji wa African Sports ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mabingwa hao watetezi walishushwa hadi nafasi ya pili mwishoni mwa wiki baada ya Simba kuifunga Mbeya City mabao 2-0 na kushika usukani kwa pointi 48 huku Yanga ikiwa na pointi 47 sawa na Azam FC kwa uwiano mzuri wa mabao ikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Iwapo Yanga itashinda mchezo wa leo itaishusha tena Simba hadi nafasi ya pili huku Azam FC ikiondolewa katika ratiba ili kuiwezesha kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika. Azam inatarajia kuondoka kesho kwenda Afrika Kusini.

Awali, Azam FC ilipangwa kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar kesho, lakini sasa mchezo huo umefutwa kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu mechi ya leo na zile za kesho.

Mchezo wa leo utakuwa wa 21 huku timu nyingine zikiwa tayari zimeshacheza isipokuwa kwa Azam, Yanga na Mtibwa Sugar na Stand United ambazo zilikuwa na viporo. Yanga inacheza na timu ambayo inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 17 na sio timu ya kudharau kwa kuwa itapambana kuhakikisha inajinasua kutoka hatari ya kushuka daraja.

Licha ya kuwa timu hiyo ya Jangwani inaweza kupewa nafasi kubwa ya ushindi, lakini huenda ikawa na kibarua kigumu cha kuondoka na pointi tatu kwani African Sports hawatakubali kufa kikondoo.
Katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa mwishoni mwa mwaka jana, Yanga iliifunga timu hiyo bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga. Hivyo, huenda timu hiyo ya Tanga ikaja na mbinu za kuwabana Yanga katika mchezo huu wa raundi ya pili na kupata matokeo mazuri kwani lolote linaweza kutokea.

Kila mmoja anahitaji ushindi kwa nafasi yake kutoka sehemu moja kwenda nyingine hivyo, huenda mchezo ukawa ni mgumu pande zote mbili kwa kuwa kila mtu atapambana kupata matokeo mazuri.

No comments:

Post a Comment