Sunday, 6 March 2016

Serikali yachunguza kampuni ya Spenkon


 
 
 
SERIKALI imesema itatoa msimamo wake kuhusu Kampuni ya Spenkon inayotekeleza mradi mkubwa wa maji katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya kujiridhisha kinachoendelea katika utekelezaji wa mradi huo.
Kauli hiyo imetolewa kutokana na madai ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuwa kampuni hiyo imefilisiwa, hivyo haiwezi kumaliza mradi huo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelo alisema hata wizara yake ina taarifa hizo ndiyo maana anafanya ziara kwenye mikoa kadhaa kuona utekelezaji wa miradi ya maji unavyokwenda.
“Ni kweli hata wizara yangu imesikia madai hayo, ila serikali inafanya ukaguzi kujiridhisha, kwa sababu hata kama kampuni hiyo imefilisiwa, lakini upo mkataba wa kisheria ambao unaelezea iwapo kampuni itashindwa kutekeleza makubaliano ndani ya mkataba huo,” alisema Kamwelo.
Alisema mradi wa maji katika mji wa Kigoma ni sehemu ya mradi wa maji mkubwa unaotekelezwa kwenye mikoa kadhaa ikiwemo mkoa wa Lindi, Kigoma na Rukwa na kwamba hivi sasa Naibu Waziri huyo yuko mkoani Lindi na Mtwara kukagua miradi ya maji ili kujiridhisha na kutoa kauli ya serikali kwa wakandarasi waliochelewesha utekelezaji wake.
Kamwelo alisema iwapo kampuni ya Spenkon imefilisiwa, sheria zipo na mkataba upo ambao pande zote mbili zitajiridhisha iwapo madai hayo ni ya kweli na kwamba sheria iliyotumika kuingia mkataba huo, itaamua jinsi ya kushughulikia suala hilo.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliitaka serikali kuvunja mkataba na Kampuni ya Spenkon inayotekeleza mradi huo wa Kigoma Ujiji, kwa madai kuwa kampuni hiyo imefilisiwa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kigoma, Zitto alisema kuwa taarifa zilizopo zinaonesha kuwa akaunti ya kampuni hiyo imezuiwa mjini London na fedha zote zinazoingia kwenye kampuni zimekuwa zikichukuliwa na makampuni yanayoidai kampuni hiyo na hivyo kuifanya kutokuwa na uwezo wa kutekeleza programu zake.
Mbunge huyo alisema kuwa awali mradi huo unaotarajiwa kugharimu kiasi cha Sh bilioni 32 ulikuwa ukamilike Machi mwaka jana, lakini wakandarasi wa kampuni ya Spenkon wakaomba iongezwe muda hadi mwezi Septemba mwaka jana, hata hivyo hawakuweza kukamilisha.

No comments:

Post a Comment