Jaji Zainab Mruke alitoa uamuzi huo katika kesi ya kupinga kuondoka katika eneo hilo, iliyofunguliwa na Juma Malumbo, Maulid Fundi, Aisha Saliko, Aisha Mhagama na wengine 99 dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilala na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Wadai hao walikuwa wanapinga kuondolewa katika eneo hilo, linalodaiwa si salama kwa makazi, pia waliomba mahakama iwazuie mkuu wa mkoa na mkurugenzi wa manispaa, wasiwahamishe katika maeneo wanayoishi na kama watahamishwa, walipwe fidia pamoja na kupewa maeneo mengine ya kuishi.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Mruke alisema baada ya kupitia ushahidi, mahakama imethibitisha kuwa watu 12 walipewa Leseni za Makazi na Manispaa ya Ilala, hivyo siyo wavamizi kwa kuwa Manispaa yenyewe ndiyo iliwaaminisha kuwa wako maeneo sahihi na wanaruhusiwa kukaa hapo.
Alisema watu hao hawataondolewa katika maneo yao mara moja, badala yake aliiamuru Manispaa hiyo iwape muda wa mwaka mmoja wa kujiandaa kuondoka hapo na pia ihakikishe inawapatia viwanja mahali pengine.
Kuhusu wadai wengine 91, mahakama ilijiridhisha na kutamka kuwa hao ni wavamizi na ikawaamuru waondoke mara moja kwa kuwa hakuna hata mmoja mwenye leseni ya makazi, kama ilivyokuwa kwa wenzao 12.
Aliongeza kuwa wadai hao hawakufika mahakamani kutoa ushahidi wao, isipokuwa wadai wanne ambao pia walitoa ushahidi kwa mambo yao wenyewe tu, “kwa sababu hawakuleta ushahidi, hakuna jambo ambalo mahakama inaweza kuamua dhidi yao”.
Jaji Mruke alisema hakuna uthibitisho wowote kuwa wakazi hao, wanakaa katika maeneo hayo kihalali, kama wenzao 12 ambao walikuwa na leseni za makazi, hivyo alisema watu ni wavamizi na wanatakiwa kuondolewa katika eneo hilo mara moja.
Alisema kama Manispaa ya Ilala itakuwa na viwanja, iwape mahali pengine lakini na kama hailazimiki kwa namna yoyote ile kuwatafutia viwanja, kwa vile hawana haki hiyo kwa sababu ni wavamizi.
Kuhusu madai ya fidia, Jaji Mruke alisema wadai wote 103, walijenga bila idhini na hakuna hata mmoja aliyekuwa na kibali cha ujenzi, hivyo walijenga kinyume cha sheria na hawana haki ya fidia yoyote.
No comments:
Post a Comment