Friday, 4 March 2016

Marais EAC waimba ‘Hapa Kazi Tu’




Mwenyekiti wa Jumuiya ya 
Afrika Mashariki (EAC), Rais John Magufuli (katikati) akiwaongoza marais wenzake wa Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Burundi na wawakilishi wa mataifa mengine kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mitambo itakayotumika katika ujenzi wa barabara ya Arusha-Holili/ Taveta-Voi yenye urefu wa kilomita 234.3 uliofanyika Tengeru, nje kidogo ya jiji la Arusha jana.
MARAIS wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wameanza kuzungumza lugha moja wakisisitizana kuchapa kazi, kuondokana migogoro ya ndani na porojo za kisiasa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo
Msimamo wa viongozi hao ulijidhihirisha jana kupitia hotuba zao kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara yenye kilometa 234.3 kutoka Arusha-Holili hadi kuingia Voi, Kenya itakayogharimu dola za Marekani milioni 353. Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na marais Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na James Wani Igga aliyemwakilisha Rais wa Sudan Kusini, Salva Kirk.
Wakiongozwa na mwenyeji wao, Rais John Magufuli, anayeongozwa na falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’ katika kuongoza Tanzania, marais Uhuru na Museveni walidhihirisha utayari wao wa kuunga mkono falsafa hiyo, kuhakikisha wanazifikisha nchi wanachama kwenye neema.
Katika hotuba yake, Magufuli aliwataka marais wenzake kujikita katika kushirikiana na kuacha tofauti za ndani kwa kuwa wananchi wanasubiri maendeleo kwa kasi ya hali ya juu. Akihimiza nchi wanachama kumaliza tofauti za ndani mwao, Magufuli alisema nchi za EAC ni tajiri ingawa kwa sasa ni masikini wa kutupwa na ombaomba.

No comments:

Post a Comment