Saturday, 12 March 2016

Matokeo ya Twiga Stars vs Zimbabwe yana funzo kubwa



Wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars wakipiga jalamba wakati wa mazoezi ya timu hiyo
 
 
NI dhahiri sasa Ligi Kuu ya soka ya wanawake inahitajika kwa udi na uvumba, hii ni kufuatia namna ambavyo timu ya soka ya wanawake ya Taifa ‘Twiga Stars’ ilivyocheza dhidi ya Zimbabwe na mambo yaliyopo nyuma ya pazia ya kiwango chao.

Twiga Stars walichabangwa mabao 2-1 pale kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, mbele ya Watanzania kwa mamia waliojitokeza kuwashangilia kwenye mchezo huo wa awali wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).
Wakicheza bila maelewano na kuonekana kutokuwa na mpango mahususi wa mechi, Twiga ‘walibahatisha’ kupata bao la kuongoza na kushindwa hata kulilinda kwa dakika tano mbele, kwani ndani ya dakika mbili Wazimbabwe walilikomboa na kipindi cha pili kuongeza la ushindi.

Tofauti ya Kiwango Kulikuwa na tofauti ya dhahiri kutoka kwenye timu zote mbili ambazo zilihusisha namna ya kucheza na wachezaji wa pande zote mbili. Twiga Stars walionekana wachovu, wasio na nguvu wala mipango mara baada ya dakika 25 za mwanzo za mchezo. Hii ni dhahiri kwamba aidha hawakuwa na mazoezi ya kutosha kuwafanya wahimili walau hata dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Inaonekana kwenye mazoezi yao mwalimu hakutilia maanani sana au kwa kiwango kinachotakiwa mazoezi ya utimamu wa mwili. Hili lilisababisha timu kucheza kwa kiwango cha chini sana kulinganisha na kipindi cha mwalimu aliyejiuzulu Rogasian Kaijage. Inawezekana bado hali ya sintofahamu ambayo ilimfanya Kaijage ajiondoe kundini bado ipo kwenye hii timu, lakini hili mwalimu alikuwa analijua wakati anapokea timu na uzuri ni kwamba yeye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Kaijage.

Inavyoonekana ameshindwa hata kuiga tu kile ambacho ‘bosi’ wake alikuwa anakifanya wakati ule kuifanya timu icheze vizuri na kwa nguvu muda wote. Kukosa pumzi kabisa Kukosa nguvu na pumzi kwa wachezaji kulifanya Twiga isiwe na ‘timu’ kiwanjani na Zimbabwe kuonekana ina timu nzuri na kutuhimili kwa kipindi chote cha dakika 90.

Ingawa ukizichambua timu zote mbili kwa wachezaji mmoja mmoja utaona kwamba kiufundi wachezaji wa Twiga walikuwa wazuri kuliko wale wa Zimbabwe, lakini ilionekana dhahiri kwamba wanategemea uwezo wa mtu binafsi kuliko muunganiko wa kitimu. Zimbabwe wao walionekana imara muda wote na wenye maandalizi ya kutosha, lakini zaidi walionekana kujua nini mahitaji yao kwenye mchezo ule na kucheza kitimu zaidi kuliko uwezo binafsi.

Walikuwa wengi kwenye kujilinda na hata wakati wa kushambulia pia kujilinda pia na kuwanyima Twiga Stars nafasi ya kuleta madhara. Zaidi ya lile bao ambalo Twiga walipata baada ya Zimbabwe kuzubaa na kuruhusu hali ya mmoja kwa moja kiwanjani, ambapo Mwanahamisi Omar aliwazidi mbio na kufunga, hawakutoa tena nafasi kama hiyo. Walihakikisha kila mara wanawazidi Twiga kwa idadi ili kupata faida ya namba ‘Numerical advantage’ iwe kwenye kujilinda ama kushambulia.
Kwa kuwa Twiga wao hawakuwa na mfumo wala mpango wa mechi, walikubali hili litokee na kila walipokwenda kushambulia walikuwa pungufu kwa idadi na mara nyingi kama sio zote walikuwa washambuliaji wawili Asha Rashidi na Mwanahamisi Omar dhidi ya mabeki wanne au watano wa Zimbabwe.

No comments:

Post a Comment