Monday, 7 March 2016

Kampuni ya utalii yamchefua Majaliwa


Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.

KAMPUNI ya uwindaji na utalii wa picha ya Mwiba Holding Limited imemchefua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutokana na madai ya kunyanyasa Watanzania na kutoa angalizo kwamba itafutiwa uwekezaji huo.
Mwiba Holding Limited inayofanya utalii wa uwindaji na picha katika Pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu katika mkoa wa Simiyu, inashutumiwa kwa vitendo vya unyanyasaji wa wananchi wanaozunguka eneo la ranchi walilolitwaa kuendesha shughuli hiyo.

Mbunge wa Meatu, Salum Khamis, alidai mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa kuwa kampuni hiyo inanyanyasa Watanzania kwa kuwateka, kuwatesa na kwamba imeingia mikataba ya ovyo yenye harufu ya rushwa na vijiji saba katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao.

Wilaya ya Meatu iliyoanzishwa Julai 1, 1987, ina ukubwa wa kilometa za mraba 8,835, na asilimia 49 ya eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za wanyamapori ambazo ni Pori la Akiba la Maswa, sehemu ya Hifadhi ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na WMA. Kutokana na madai hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Eraston Mbwilo, kuchunguza madai hayo na ifikapo Ijumaa wiki hii, awe amempa ripoti.

“Leo (juzi) ni tarehe tano… Hadi tarehe kumi na moja nipate ripoti. Ikibidi waondoe, siyo lazima abaki yeye. Mwekezaji lazima afuate masharti, kama sivyo afutwe aondoke. Huo mwiba utamchoma mwenyewe,” aliongeza Waziri Mkuu huku akishangiliwa na wananchi wa Meatu.

Katika maelezo yake baadaye kwa gazeti hili, Mbunge Salum alidai kuwa Mwiba Holding Limited na kampuni dada ya TGT imemilikishwa hekta 12,000 katika kijiji cha Makao kwa ushirikiano na Halmashauri, na kupewa ranchi ambayo ilikuwa inategemewa na wananchi kwa kilimo na mifugo.
Aidha, alisema vijiji vya Mwangudo, Irambandogo, Sungu, Mbushi, Lukale na Sapa vimejumuishwa katika WMA na wawekezaji hao kuchukua hekta 29,000 na kuingia mkataba mwingine na kijiji cha Mwangudo na kupewa hekta nyingine 79,000.

Alidai kuwa wawekezaji hao wanatumia askari wao wanaolipwa mishahara, na kwamba katika mikataba hiyo, Halmashauri inalipwa Sh milioni 40 kwa mwaka na kijiji cha Makao Sh milioni 24, fedha alizoeleza kuwa ni ndogo kulinganisha na mapato ya Mwiba inayomiliki hoteli ya nyota tano katika eneo hilo.

Alivitaja vitendo vya unyanyasaji vinavyofanyika kuwa ni pamoja na mifugo kufukuzwa kwa kutumia helikopta na kuingizwa makorongoni pamoja na askari wake kuwafuata wananchi umbali wa kilometa 50 na kuwatesa.
Akizungumzia tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga alisema kwa kuwa Waziri Mkuu amemwagiza Mkuu wa Mkoa kufanya uchunguzi, ni vyema wao wakasubiri uchunguzi huo na kama kutakuwa na jukumu linalowataka kulifanya, watafanya hivyo.

No comments:

Post a Comment