Monday, 28 March 2016

Shein aitisha Baraza la Wawakilishi


 

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ameitisha mkutano wa kwanza wa Baraza jipya la Tisa la Wawakilishi keshokutwa kwenye Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani mjini Unguja.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Dk Yahya Khamis Hamad wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi jana.

Hamad alisema amepokea barua kutoka kwa Rais Shein ambayo inaitisha mkutano wa kwanza wa Baraza la Wawakilishi, ambalo kwa mujibu wa kanuni zake, linamtambua Rais kama ni sehemu ya pili ya baraza hilo na ndiyo mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na mahala pa kufanyika mkutano wa kwanza.

Alisema kama Kanuni za Baraza la Wawakilishi Toleo la 2012 linaelezea kuwa katika Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Wawakilishi shughuli ya mwanzo ni kumchagua Spika wa Baraza la Wawakilishi, na hadi sasa aliyeteuliwa na kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ambaye amethibitishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni Zuber Ali Maulid kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katibu wa Baraza la Wawakilishi alisema wajumbe wote wameanza kujengewa mazoea ikiwa pamoja na kujisajili kuanzia leo hadi Aprili 6, mwaka huu. “Kesho (leo) kusajiliwa kwa wajumbe na kupigwa picha za vitambulisho, Machi 29 asubuhi kutakuwa na mkutano wa vyama vya siasa, pia siku hiyo mchana kutakuwa na mkutano wa mwanzo wa wajumbe wote wa baraza, Machi 30 kuanza kwa mkutano wa kwanza wa baraza na baadaye uchaguzi wa spika pamoja na kiapo cha spika na wajumbe,” alisema Hamad.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa Machi 31, mwaka huu kutakuwa na uchaguzi wa Naibu Spika na Mwenyekiti wa Baraza, Aprili 5, 2016 kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe wa Tume ya Bajeti ya Baraza na wajumbe watano wa baraza watakaoingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baraza hilo jipya linalotarajiwa kuanza keshokutwa litakalohutubiwa na Dk Shein lina idadi ya wajumbe 88 ambao wajumbe 54 ni wawakilishi waliochaguliwa na wananchi, 22 Wawakilishi wa Viti Maalumu, 10 uteuzi wa Rais ambao bado kuteuliwa, Mjumbe mmoja ambaye ni Mwanasheria Mkuu na Spika ambaye ni nje ya wajumbe wa baraza.

No comments:

Post a Comment