Yanga ilienguliwa kileleni Jumapili baada ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, hivyo Simba kufikisha pointi 48 na kuiacha Yanga nafasi ya pili ikiwa na pointi 47 na Azam nafasi ya tatu ikiwa na pointi kama hizo isipokuwa ilikuwa inatofautiana na Yanga uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kutokana na ushindi huo wa jana, Yanga imefikisha pointi 50 ikiongoza ligi ikifuatiwa na Simba yenye pointi 48 na Azam pointi 47. Hata hivyo, Simba inaweza kurejea kileleni kama itashinda mchezo wake wa kesho wa ligi hiyo dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba na Yanga zote zimecheza mechi 21 hadi sasa, wakati Azam imecheza mechi 20. Ushindi huo wa Yanga pia ni salamu tosha kwa wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, APR ya Rwanda itakayokutana nayo Jumamosi wiki hii mjini Kigali, Rwanda.
Katika mchezo huo, Yanga ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 33 mfungaji akiwa Kelvin Yondani kwa shuti kali, kisha dakika nne baadaye Donald Ngoma aliifungia Yanga bao la pili akiunganisha krosi ya Juma Abdul.
Yanga ingeweza kwenda mapumziko ikiwa na idadi kubwa ya mabao kama nafasi ilizopata zingetumiwa vyema na Deus Kaseje, Ngoma na Amis Tambwe, wakati washambuliaji wa Sports nao walikosa umakini walipokaribia lango la Yanga.
Dakika ya 50 Tambwe aliifungia Yanga bao la tatu katika mchezo huo, likiwa ni la 16 kwake katika ligi hiyo na kufikisha idadi sawa na yale aliyofunga mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza ambaye hadi jana alikuwa akiongoza katika ufungaji akiwa na mabao 16.
Yanga waliendelea kushangilia mabao, baada ya Matheo Simon kufunga bao la nne dakika ya 59 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Haji Mwinyi ikiwa ni dakika ya tatu tu tangu aingie kuchukua nafasi ya Ngoma.
Tambwe alipachika bao la tano dakika ya 72 likiwa ni bao lake la 17 katika ligi hiyo msimu huu na hivyo kumpiku Kiiza na kushika usukani katika ufungaji. Tofauti na ilivyokuwa kipindi cha kwanza, ambapo washambuliaji wa Sports walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza, hali ilikuwa tofauti kipindi cha pili na kuonekana timu hiyo kuzidiwa kimchezo.
No comments:
Post a Comment