Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alitoa taarifa hiyo ya mwelekeo huo ikiwa tayari mvua za masika zimeanza kunyesha maeneo mbalimbali nchini ikiwemo jijini Dar es Salaam.
“Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi 2016 katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria na kusambaa katika maeneo mengine yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka,” alisema Dk Kijazi.
Aidha mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Hata hivyo maeneo machache yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Mvua za msimu zinazoendelea zinatarajiwa kunyesha katika kiwango cha wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi.
TMA ilieleza kuwa kunyesha kwa mvua hizo ni faraja kwa wafugaji, kwani upatikanaji wa malisho unatarajiwa kuwa wa kuridhisha hususan katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria na Nyanda za juu kaskazini Mashariki.
Pia wakulima wa maeneo yote ambayo mvua hizo zitanyesha zitasaidia kuwepo kwa hali ya unyevunyevu wa udongo na kuwa ya kutosheleza shughuli za kilimo katika maeneo mengi. Hata hivyo, mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa kunyesha zinaweza kusababisha hali ya unyevunyevu wa udongo kupita kiasi hivyo kuathiri mazao.
TMA pia ilisema mlipuko wa magonjwa kama vile Malaria unatarajiwa kujitokeza baada ya kunyesha kwa mvua hizo huku vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha mafuriko. Mamlaka za miji nchini zimetakiwa kuchukua tahadhari, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya maji taka huku mamlaka za afya zikitakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya milipuko ya magonjwa.
No comments:
Post a Comment