Saturday, 12 March 2016

Yanga, Azam kazini leo



Mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima.


YANGA na Azam kazi  leo. Wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), leo wanashuka viwanjani ugenini katika mashindano tofauti kusaka pointi.

Yanga itakuwa mgeni wa APR kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, Rwanda huku Azam FC pia ikiwa mgeni wa Bidvest Wits kwenye Uwanja wa Bidvset nchini Afrika Kusini. Yanga, mabingwa wa Tanzania Bara, watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 3-0 nchini humo walipokutana kwa mara ya kwanza na APR mwaka 1996.

APR yenye wachezaji wengi wa timu ya Taifa ya Rwanda sio timu ya kuidharau, kwani iliwahi kuitoa Yanga katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo mwaka huo kwa jumla ya mabao 3-1 ikishinda 3-0 kwao na ule wa marudiano uliochezwa Dar es Salaam Yanga ikishinda bao 1-0. Timu hizo zimekuwa zikitambiana kupata ushindi kutokana na jinsi ambavyo kila mmoja amekuwa akifanya vizuri katika ligi yake.

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm kabla ya kuwasili Rwanda, alisema atawaandaa wachezaji wake kisaikolojia na kimashindano kuhakikisha wanapata ushindi ugenini ili kutengeneza mazingira mazuri ya mchezo wa marudiano utakaochezwa baada ya wiki moja. Yanga ilivuka raundi hiyo baada ya kuitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0.

Wakati huo huo, habari zilizopatikana kutoka Kigali, Rwanda jana zilisema kuwa kiungo nyota wa Yanga, Haruna Niyonzima amekuwa gumzo kubwa kuhusu mchezo huo. Niyonzima aliyejiunga na Yanga msimu wa mwaka 2011/12 akitokea APR ya Rwanda anaelezwa kuwa ni mchezaji anayependwa kuliko wote miongoni mwa mashabiki wa soka wa Kigali, Rwanda, hasa kuelekea mchezo wa leo.

Kwenye mazoezi ya Yanga yaliyofanyika juzi na jana, mashabiki walifurika uwanjani na gumzo kubwa likiwa ni Niyonzima. “Amepokelewa kwa shangwe sana na jana kwenye mazoezi yetu mashabiki walifurika sana kumuangalia, anapendwa sana hapa Kigali,” alisema Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh.

Mbali na Niyonzima, mashabiki wa APR wamekuwa wakiulizia mara kwa mara taarifa za wachezaji kama vile Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amis Tambwe na winga Simoni Msuva wanaowachukulia kama ni hatari kwao kuelekea mchezo huo.

”Wana taarifa za akina Ngoma, Tambwe, Kamusoko na Msuva ambao kwao wanawachukulia ni hatari sana kuelekea mechi hiyo, mazungumzo na maswali yao ni juu ya hawa jamaa, wameanza kuingiwa hofu hasa wakisikia habari juu ya viwango vyao,” alisema Saleh.

Saleh alisema kwamba wachezaji wote wako kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huo isipokuwa kiungo Saidi Makapu anayesumbuliwa kifua na mafua. Wakati huo huo, akizungumzia mchezo huo Niyonzima alisema ana imani leo Yanga itaibuka na ushindi mnono.

“Anayekwambia mchezaji ana mapenzi na timu, huyo anakudanganya, nilicheza APR lakini kwa sasa nipo Yanga na ndipo kazini kwangu, siwezi kucheza kwa mapenzi kwenye mechi hiyo eti kwa sababu nilikuwa APR, nitaonesha uwezo wangu wote na nikipata nafasi ya kuwafunga nitawafunga,” alisema Niyonzima.

Hata hivyo, aliwaonya wachezaji wenzake kujituma kwani japo APR inaundwa na wachezaji wengi chipukizi kwa sasa ni timu nzuri inayoweza kufanya chochote kwenye mechi yoyote na hivyo haitakuwa mechi rahisi.

Kwa upande wa Azam FC wanakutana na Bidvest kwa mara ya kwanza, hivyo ni timu zisizofahamiana, lakini kila moja huenda ikacheza kwa tahadhari kutokana na kusomana mapema.
Wakati Azam FC ikianzia raundi hiyo ya kwanza, Bidvest Wits imefika hatua hiyo baada ya kuiondosha Light Stars ya Shelisheli kwa mabao 9-0, ikianza kwa kushinda ugenini 3-0 kabla ya kuichapa tena 6-0 nyumbani. Kocha Msaidizi wa Azam, FC Mario Marinica, alisema wameiona Bidvest Wits kwenye mechi kadhaa na wanajua mbinu wanazotumia na kwamba wanayo nafasi nzuri ya kuwatoa Wasauzi hao.

“Tunauchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa, hata wapinzani wetu nao tunawachukulia kwa uzito mkubwa, tayari tumeshawapeleleza kwenye mechi kadhaa, tunajua ubora wao na ni timu nzuri, ila sisi tuko kamili na tayari kucheza nao,” alisema.

Naye mshambuliaji wa Azam FC, Allan Wanga amesema kuwa anaweza kuifunga Bidvest Wits ya Afrika Kusini, endapo atapewa nafasi ya kucheza leo. Kwa mujibu wa tovuti ya Azam, Wanga anajipa matumaini hayo kutokana na kuijua vema Bidvest Wits baada ya kufanya majaribio ya wiki mbili Juni mwaka jana, kabla ya kutua Azam FC.

“Nilikuwa mwezi wa sita mwaka jana hapa Bidvest Wits nikafanya vizuri kwa wiki mbili kwa sababu walitaka kunisaini nikiwa El Merreikh tangu miaka miwili iliyopita baada ya mazoezi ikawa wamekubaliana na wakala wangu ili kunisajili, lakini wakati huo mama yangu (marehemu) alikuwa amezidiwa na ugonjwa na kibali changu cha kazi hapa kilikuwa hakijatoka,” alisema.
Nyota huyo wa kimataifa kutoka Kenya, alizungumzia aina ya soka wanalocheza Bidvest Wits na kudai kuwa timu hiyo haichezi soka la pasi kama zilivyo timu nyingine huko Afrika Kusini bali hucheza zaidi mipira mirefu.

No comments:

Post a Comment