Sunday, 6 March 2016

Viwanda vya kusokota nyuzi kuongeza bei ya pamba

Pamba

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema njia pekee ya kupandisha bei ya pamba nchini ni kujenga viwanda vya kusokota nyuzi ili kuinua thamani ya zao hilo

Alisema chini ya uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, hilo litawezekana na hasa kutokana na kuwapo kwa mizengwe katika zao la pamba nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Michezo wa Mwamapalala wilayani Itilima katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku sita mkoani Simiyu juzi.

Majaliwa alikiri kuwa bei ya pamba inabadilika kutokana na bei katika soko la dunia, ambako kuna wazalishaji mbalimbali, lakini kitakachookoa hali hiyo ni kuwapo kwa viwanda vya kusokota nyuzi nchini ambavyo vitasaidia kuongeza thamani ya zao hilo.

“Bei ya pamba huwa inabadilika katika soko la dunia, hivyo kusababisha bei hiyo kuporomoka hadi hapa nchini. Huku kwenu kuna michezo michezo katika bei ya zao hilo,”alisema Waziri Mkuu na kuongeza. “Nitarudi kutoa mwongozo kuhusu suala hili, nimeagiza kuwapo kwa kikao cha watu wa Bodi ya Pamba. Kuna mizengwe mizengwe sana katika suala hili. Mazao ya pamba, korosho na kahawa yamekuwa hayaendeshwi vizuri. Tatizo ni mfumo. Ushirika unatuumiza zaidi,” alisema kwa msingi huo, njia pekee ya kupandisha bei ya pamba ni kwa kujenga viwanda vya kusokota nyuzi ambavyo vitafanya uzalishaji wa nguo ufanyike nchini hivyo kuuzabidhaa nje.

Aliwaahidi wananchi wa Itilima, Simiyu na Tanzania kwa ujumla kuwa serikali italifanyia kazi suala hilo la bei ya pamba na kuja na ufumbuzi wa kudumu.

Waziri Mkuu alilazimika kulitolea ufafanuzi suala hilo baada ya wabunge wawili wa Viti Maalumu, Esther Midimu (CCM) na Gimbi Masaba (Chadema), kueleza masikitiko yao kuhusu kuporomoka kwa bei ya pamba katika soko la ndani.

Wakati akijinadi kuomba ridhaa ya Watanzania kumchagua kuwa Rais, Dk John Magufuli aliahidi kuwa Tanzania itakuwa nchi ya viwanda chini ya utawala wake, na hivyo kuipeleka katika nchi zenye uchumi wa kati.

Aidha, Waziri Mkuu aliwaambia wananchi hao wa Itilima kuwa ahadi ya Rais Magufuli ya kujenga barabara ya lami kutoka Busega – Bariadi – Itilima – Meatu na kuunganishwa na wilaya ya Mkalama mkoani Singida iko na pale pale naitatekekezwa

No comments:

Post a Comment