Pia, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imepokea maombi ya Shirika la Umeme (Tanesco) ya kushusha bei ya umeme kwa asilimia 1.1 na kuondoa kabisa gharama za maombi ya awali ya wateja wapya na gharama za huduma kwa wateja wa majumbani .
Aidha, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo, amepiga marufuku Tanesco, kununua transfoma kutoka nje ya nchi na badala yake imetakiwa kununua za kiwanda cha hapa nchini.
Kuhusu kushusha bei
Baada ya kupokea maombi hayo ya Tanesco, Ewura imeanza mchakato wa kupata maoni ya wadau ili kujua uhalali wa maombi hayo ya mapendekezo ya bei za huduma hiyo.
Imewataka wadau wote kuhudhuria mkutano wa kukusanya maoni, utakaofanyika kesho kutwa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema walipokea maombi ya Tanesco Februari 24, mwaka huu ya kutaka mabadiliko ya bei ya umeme kwa miaka miwili kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.
Maombi yaliyowasilishwa yanajulikana kama gharama za fomu ambazo ni Sh 5,900 na gharama za huduma (service charges) ni Sh 5,520 kwa mwezi kwa wateja wa majumbani.
Akijibu maombi hayo, Ngamlagosi alisema Sheria ya Umeme Namba 131 Kifungu Namba 24(2) kinaitaka Mamlaka kufanya mabadiliko ya bei, zinazotozwa na mtoa huduma mara moja kila baada ya miaka mitatu.
Pendekezo la wastani wa badiliko la bei za umeme ni asilimia 1.1 kuanzia Aprili Mosi mwaka huu na asilimia 7.9 kuanzia Januari Mosi mwakani.
Ngamlagosi alisema maombi hayo yamefika na wao wameanza mchakato wa kupata maoni ya wadau ili kufahamu uhalali wa mambo hayo na kuwataka wadau wote wa umeme kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano utakaofanyika kesho kutwa, Dar es Salaam ili watoe maoni yao.
“Mkutano wa wadau kukusanya maoni kuhusu maombi ya Tanesco utafanyika Machi, 4, mwaka huu, aidha wale wanaopenda kutoa maoni kwa maandishi tunaomba wafanye hivyo na kuyatuma Ewura ndani ya wiki mbili kuanzia leo”, alisema Ngamlagosi.
Awali Februari 29, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felichesmi Mramba alisema wamewasilisha maombi hayo Ewura baada ya Tanesco kufanya tathmini ya kina kimahesabu na kubuni namna ambayo wateja wao wataweza kupata ahueni ya gharama kwa kuzingatia mazingira ya sasa.
Alisema punguzo hilo la asilimia 1.1 ni kwa mwaka wa kwanza na matarajio ni kwamba mwaka wa pili, watapunguza kwa asilimia 7.9.
Bei elekezi ya mafuta
Katika hatua nyingine, Ewura imetangaza bei elekezi za mafuta ya aina zote, itakayoanza kutumika kuanzia leo, inayoonesha kupungua kwa bei hiyo ukilinganisha na mwezi uliopita.
Katika bei elekezi hiyo, mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya taa yamepungua bei kwa Sh 31 sawa na asilimia 1.70 ukilinganisha na bei iliyopita iliyokuwa Sh 34.36 sawa na asilimia 1.98.
Akizungumzia kupungua kwa bei hiyo, Ngamlagosi alisema hiyo imetokana na bei ya mafuta kwenye Soko la Dunia kushuka.
Alisema kwamba katika mabadiliko hayo, bei za mafuta kwa mkoa wa Tanga, zitabaki zile zile za mwezi uliopita, hiyo ni kwa sababu hakuna mafuta mapya yaliyopokelewa kwenye bandari ya Tanga.
Aidha, Ewura imezindua huduma ya kujua bei elekezi za mafuta kwa kutumia ujumbe wa siku ya mkononi kwa kupiga namba *152*#, kisha kufuata maelekezo na kwamba huduma hiyo ni ya bure na inapatikana kwenye mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.
Ununuzi wa transfoma
Veronica Mheta kutoka Arusha anaripoti kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo, amepiga marufuku Shirika la Umeme Tanzania, (Tanesco), kununua transfoma toka nje ya nchi na badala yake ametaka linunue za kiwanda cha kutengeneza transfoma cha Tanelec, ambako Tanesco wanamiliki hisa asilimia 20.
Akizungumza jijini Arusha jana katika kiwanda cha Tanelec, Profesa Muhongo alisema inasikitisha kuona shirika hilo linaacha kununua mali yake na kukimbilia mali za nje, kwa kigezo tu cha sheria ya manunuzi ya umma zinawabana.
“Kuanzia sasa acheni kabisa kuagiza transfoma za nje na mchukue za kwenu ambako mnamiliki hisa asilimia 20 na ukiweka hisa za Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) wanaomiliki asilimia 10, zinakuwa hisa asilimia 30, halafu mnakimbilia nje,” alisema
No comments:
Post a Comment