Tuesday, 8 March 2016

Wafanyakazi 800 NIDA kikaangoni



Waziri Kitwanga alipokutana na wafanyakazi wa NIDA


MAMLAKA ya Taifa ya Utambulisho (NIDA) imetangaza kusitisha mikataba ya wafanyakazi 597 wa muda kutokana na uzalishaji kuwa chini ya ufanisi, usioendana na idadi ya wafanyakazi walio nao.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk Modest Kipilimba, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kwamba pia wafanyakazi 802 wa kudumu ilionao, inaendelea kuwafanyia tathmini pia iwapunguze na kuwarudisha Utumishi wapangiwe kazi nyingine. Akizungumzia wafanyakazi hao wa muda, Dk Kipilima alisema, watafuata taratibu za mikataba yao kabla ya kumalizana nao huku akisisitiza hawatawaacha ‘kijuu juu’.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi, mamlaka imekuwa ikizalisha vitambulisho 1,200 kwa siku badala ya 24, 000 kwa siku, jambo alilosema wanazalisha chini ya asilimia 10 hivyo kusababisha hasara kwa mamlaka. Alisisitiza kuwa wafanyakazi hao wanapunguzwa kwa sababu ya kutokuwapo kazi ya kuwapa. Alisema wanachofanya, ni kutaka kujipanga upya kuhakikisha ufanisi wa mamlaka hiyo unaongezeka.
Vilevile alisema, hata hao wafanyakazi wa kudumu, wanatakiwa kufanya kazi kwa ufanisi mamlaka ifikie lengo ambalo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata utambulisho wa taifa kabla ya Desemba 31, mwaka huu. Aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kuhakikisha wanafikia lengo. Wakati huo huo alisema ipo mikataba mingi na mingine ni ya thamani kubwa, hivyo wanafanya kuipitia upya kujiridhisha kama ilifuata sheria.
Alitoa mfano wa mikataba ya wafanyakazi na mingine waliyoingia na kampuni mbalimbali. Alisema ikibainika kuwapo mikataba ambayo haikufuata sheria, itavunjwa. Alizungumzia pia mashine za BVR na kusema baada ya uchaguzi, zilikuwa zinafanyiwa matengenezo na sasa wanatarajia kupokea mashine 5,000 kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Alisema mashine hizo zitasaidia kuongeza kasi ya kufikia wananchi wengi na kuwapa vitambulisho.
Alisema vitambulisho vya mpiga kura ni tofauti na vya Nida ambavyo vina mchakato mrefu. Kuhusu wataalamu watakaotumia mashine hizo, alisema wakizipata, wataangalia idadi ya wanaohitajika na ni kwa muda gani ili kuzuia watu kupewa mikataba ambayo kazi ikiisha, wanaendelea kulipwa bila kazi. Alisema lengo ni kuondokana na dhana kwamba watu wanalipwa kwa sababu wameajiriwa, bali walipwe kwa sababu wanafanya kazi.

Alisema kulingana na mahitaji ambayo yanahusu mahitaji ya watumishi na bajeti, kwa hali ya sasa ya Nida hawana bajeti ya kuendelea kulipa wafanyakazi hao wa mikataba. Alisema yapo mabadiliko ya mpango kazi wa mamlaka ambao kwa sasa hatua zote za usajili zitafanyika katika ngazi zote za wilaya. Alisema sasa watumishi watakaokuwepo, watakuwa katika ofisi za manispaa badala ya kupanga au kuweka kambi maeneo ya wazi.

Hivyo alisema, watumishi waliopo kwa masharti ya kudumu wanakidhi kuendelea kutekeleza kazi iliyokusudiwa ngazi za wilaya kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji na mitaa. Alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa mpango wa mamlaka wa kurekebisha maeneo yanayohitaji mabadiliko makubwa kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu.

Akizungumzia kukosekana saini kwenye vitambulisho vya taifa, alisema ili ziwepo kwenye vitambulisho vingine vipya, ni lazima kanuni zibadilishwe. Alisema wameshaanza mchakato wa kurekebisha hizo kanuni na kwamba zikikamilika, watapeleka kwa Katibu Mkuu na baadaye kwa Waziri mwenye dhamana na taasisi hiyo zipitishwe. Hata hivyo alisema vitambulisho vya sasa, saini zake ziko kwenye kanzidata ambazo si rahisi kuonekana wazi.

No comments:

Post a Comment