Wednesday, 2 March 2016

Gesi nyingi yapatikana mkoani Pwani




Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio

WAKATI Tanzania ikiendelea kunufaika na ugunduzi wa gesi asilia, ambayo imeshaanza kutumika kufua asilimia 70 ya umeme unaotumika nchini, ugunduzi mwingine mkubwa wa gesi kuwahi kutokea nchi kavu, umefanyika na kuthibitishwa katika mkoa wa Pwani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika mitambo ya kuchakata na kusafirisha gesi ya Madimba, mkoani Mtwara, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Mataragio, alisema wiki iliyopita kulifanyika ugunduzi wa gesi nyingine, futi za ujazo trilioni 2.17.
Kwa mujibu wa Dk Mataragio, ugunduzi huo uliofanyika katika Kitalu cha Ruvu, ni mbali na ugunduzi uliokuwa umeshafanyika wa futi za ujazo trilioni 55.08 katika kina cha bahari na nchi kavu.
Kuhusu gesi ya Ruvu, alisema anazo taarifa zinazoonesha kwamba kuna gesi nyingi katika Bonde la Ruvu, ambako ndio eneo pekee la nchi kavu lenye gesi nyingi hapa nchini na kuongeza hiyo ndio tija anayoizungumzia.
Kuhusu mitambo hiyo ya Madimba, Dk Mataragio alisema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2011, ukiwa na sehemu kuu tatu ambazo ni; ujenzi wa bomba la inchi 36 kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, Dar es Salaam, ujenzi wa mitambo hiyo ya kuchakata gesi asilia Madimba na mitambo mingine Songo Songo.
Kwa mujibu wa Dk Mataragio, gharama za mradi huo hadi sasa ni takribani Dola za Marekani bilioni 1.2, ambazo kati ya hizo asilimia tano ni mchango wa Serikali na nyingine ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Exim Bank ya China.
Pamoja na gharama hizo, Dk Mataragio alisema matumizi ya gesi asilia iliyotokana na mradi huo katika kufua umeme, yameokoa matumizi ya fedha za kigeni takribani Dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka, ambazo zilikuwa zitumike kununulia mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sasa tunazalisha wastani wa futi za ujazo milioni 45-50 kwa siku (mmscfd) hapa Madimba. Hata hivyo uwezo wetu ni kuzalisha futi za ujazo milioni 130 kwa siku (mmscfd) kutoka katika visima vitano vya gesi asilia vilivyopo eneo la Mnazi Bay,” alisema.
Akizungumza baada ya kuelezwa kuhusu utendaji wa mitambo hiyo na faida yake kwa Taifa, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema pamoja na mafanikio ya sasa ya kuwasha umme kwa kutumia gesi asilia, ni lazima gesi ipelekwe kwa wananchi kwa ajili ya matumizi ya majumbani

No comments:

Post a Comment