Monday, 7 March 2016

Pluijm awalaumu wachezaji wake




Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Van Pluijm
 
KOCHA wa Yanga Hans Pluijm amesema hana furaha na matokeo ya sare aliyopata katika mchezo dhidi ya Azam FC kwa kuwa wachezaji wake waliendelea na tatizo la kupoteza nafasi za wazi. Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam juzi, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na kuendelea kufanana kwa pointi sawa 47.

Akizungumza baada ya mchezo huo Pluijm alisema matokeo hayo huenda yalifurahiwa na Azam FC lakini kwake, hakuridhishwa nayo, kwani walikuwa na kila sababu ya kushinda kutokana na nafasi kadhaa walizopata lakini kushindwa kuzitumia.
“Azam wanaweza wakawa wanafurahia matokeo haya, lakini upande wangu mimi siyafurahii kwa sababu tulitengeneza nafasi nyingi, tumeshindwa kuzitumia na tulikuwa na kila sababu ya kushinda kutokana na nafasi tulizotengeneza,” alisema.
Pamoja na hilo, awali kabla ya Pluijm kuzungumzia mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC Denis Kitambi alimlalamikia mwamuzi wa mchezo huo kwa kushindwa kuwapa penalti baada ya Kelvin Yondani kuanguka mbele ya Jonh Bocco aliyekuwa akitaka kufunga.
Hatahivyo, Pluijm aliijia juu klabu hiyo na kusema Yondani ndio aliyeangushwa na Bocco hivyo, sio kwamba timu ilibebwa na mwamuzi kama ambavyo Kitambi alilalamika na kumtaka kabla ya kutoa malalamiko hayo kwenda kuangalia mechi vizuri kwenye televisheni.
Kitambi alisema anaamini kikosi chake kina wachezaji wazuri kuliko cha Yanga ndio maana katika michezo yao mitano wanatoka suluhu huku akiwatupia lawama waamuzi wa mchezo huo kwa kuamini mara zote huwabeba Yanga.
“Waamuzi wamekuwa wakiibeba Yanga, lakini sisi tuna timu bora, lazima tuipongeze timu yetu kwa kupambana hadi dakika za mwisho,” alisema. Kitambi aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri huku akikiri licha ya ugumu wa mchezo huo walipambana hadi dakika za mwisho.
Alisema dakika 25 za kwanza kikosi hicho kilianza vizuri na baadaye kuonekana kupotea hali iliyosababisha kuzungumza na wachezaji wao baada ya mapumziko na kupata matokeo hayo.

No comments:

Post a Comment