Monday, 7 March 2016

MANULA ASEMA MGUSO WA WAWA ULIMPOTEZA MABOYA JUMA ABDUL AKAWAFUNGA

MANULA


 
 
 
 
 
 
 
 
 
Kipa wa Azam FC, Aishi Manula, ameweka wazi kuwa asingefungwa bao la kwanza na Juma Abdul wa Yanga kwa shuti kali aliloliachia nje ya 18 na kutinga wavuni kama si beki wao, Muivory Coast, Pascal Wawa kusaidia 
shambulizi hilo.

Manula ameeleza kuwa ni kweli shuti lile ambalo lilibadili matokeo na kuwa 1-1 kabla ya mchezo huo baadaye kumalizika kwa 2-2, lilikuwa kali lakini alishapiga mahesabu sahihi ya kuliokoa isipokuwa Wawa ndiye aliugusa na kumpotezea mahesabu yake hayo.

“Unajua pale nilishapanga kuuokoa ule mpira na niliuona kwamba unakwenda wapi lakini ghafla Wawa akaugusa bahati mbaya, kwa hiyo ukapoteza muelekeo na kwenda kinyume na mahesabu niliyokuwa nimeshayapanga kuuokoa.

“Kama si Wawa ule mpira ningeuficha, ila niseme tu hata Juma naye alifanya kazi nzuri kwa mpira namna alivyoupiga. Kiujumla mchezo ulikuwa wa kiushindani na si mbaya hata hii pointi moja tumechukua, tunazidi kupambana kwa ajili ya michezo mingine. Ligi bado mbichi,” alisema Manula.
 
Matokeo ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ulizifanya Yanga na Azam kuendelea kufungana kileleni kwa pointi 47, wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa. Matokeo ya ushindi kwa Simba katika mechi ya jana dhidi ya Mbeya City yangeweza kuwaweka kileleni kwa pointi 48.

No comments:

Post a Comment