Friday, 11 March 2016

Sudan Kusini yatakiwa kuimarisha usalama




Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir.
 
BUNGE la Afrika Mashariki (EALA), limemtaka mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sudan Kusini kusaini haraka mkataba wa kutawazwa kuwa mwanachama kamili na kuhakikisha anaimarisha amani na usalama ndani ya mipaka yake.

Aidha, Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa ya mwanachama huyo mpya kwa kufanya biashara na kuongeza masoko. Wakipitisha azimio la kuipongeza Sudan Kusini baada ya hoja iliyotolewa na Mbunge Peter Mathuki (Kenya) na kuungwa mkono na Mbunge Dora Byamukama (Uganda), wabunge hao wamepongeza hatua hiyo na kusema itasaidia kuongeza soko la jumuiya.
Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliokutana wiki iliyopita mjini Arusha, walipokea taarifa ya Baraza la Mawaziri wa EAC na kuikubalia Sudan Kusini kuwa mwanachama. Akiwasilisha hoja, Mathuki alisema hatua ya Sudan Kusini kujiunga na EAC kutasaidia kupanuka na kuongeza uwezo wa umoja wa kanda yenye wananchi wapatao milioni 160.
Pia itasaidia kukuza biashara na maendeleo ya uchumi kwa ujumla hasa katika kuelekea kujenga Umoja wa Afrika. Akichangia hoja, Mbunge Shyrose Bhanji (Tanzania) alitoa mwito kwa Serikali ya Sudan Kusini kuhakikisha amani na usalama wa raia wake wote ili waweze kuvuna faida za utengamano.

“Ni vyema mwananchi wa EAC, hususan wa Tanzania kutumia fursa za Sudan Kusini ambao ni wazalishaji wa mafuta kwa kufanya biashara na kupanua masoko,” alisema. Naye Mathuki aliwapongeza wakuu wa EAC kwa kuiingiza Sudan Kusini katika muda muafaka na kusisitiza kuwa ni muhimu kwa mwanachama huyo mpya kuzingatia kanuni zote za mkataba wa EAC.

“Kwa Sudan Kusini kujiunga na jumuiya kuna manufaa makubwa kwa umoja huo,” alisema Dora Byamukama na kutolea mfano maeneo ya rutuba na yenye utajiri ambao ni muhimu kwa mchakato wa utengamano.
Mbunge Judith Pareno (Kenya) alisema kuingia kwa Sudan Kusini katika EAC ni ishara ya muungano wa familia hiyo iliyokuwa imetengwa kutokana na mipaka ya wakoloni. Naye Hafsa Mossi (Burundi) alipongeza uongozi wa Sudan Kusini kwa kuwa na mawazo na kufanya bidii kujiunga na EAC mara baada ya kupata uhuru.

“Hakuna muda bora kwao (Sudan Kusini) kujiunga na EAC. Nimefurahi sana kuona maendeleo ambayo ni dhahiri yataongeza thamani ya jumuiya”, alisema. Alisema kuwa jumuiya imeonesha dhamira yake ya dhati ya kuleta amani na hivi karibuni yalisainiwa makubaliano ya kuihakikishia Sudan Kusini yaliyosainiwa Tanzania.

Naye Abubakar Ogle (Kenya) alisema ni muhimu kwa EAC kuzingatia kanuni zote ikiwa ni pamoja na utawala wa sheria na utawala bora katika kipindi chote. “Tusibaki kujikita katika kuangalia namna ya kukuza masoko na kukuza uchumi, lazima kuzingatia utawala wa sheria na utawala bora, tusipofanya hivi umoja huu utabaki kuwa wa kutatua mgogoro,” alisema.

Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Richard Sezibera alisema Sudan Kusini waliomba kujiunga na EAC katika msingi wa mchakato wa kuingizwa kuharakishwa na kwamba uwezo wa nchi ulikwenda mbali zaidi ya uhakiki. “Tumefanya kazi pamoja katika kuimarisha uwezo katika masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya ukusanyaji mapato na utawala wa forodha,” alisema.

No comments:

Post a Comment