Wednesday, 2 March 2016

Mayanja aitangazia maumivu Mbeya City





Kocha wa Simba, Jackson Mayanja

JACKSON Mayanja, kocha wa Simba amesema ana uhakika kwa asilimia 100, kikosi chake Jumapili kitaibuka na ushindi mbele ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Mganda huyo alisema sababu ya kujiamini huko ni kutokana na maandalizi mazuri wanayoendelea nayo kambini Morogoro pamoja na wachezaji wake kuimarika kimawazo baada ya ushindi wa 5-1, dhidi ya Singida United kwenye kombe la FA.
“Ilikuwa ni bahati mbaya na makosa madogo madogo ndiyo maana tukapoteza mchezo na Yanga, lakini kwasasa tupo vizuri na hatutapenda kurudia makosa tena na tumejipanga kuwafunga Mbeya City Jumapili na hilo nina uhakika nalo kutokana na utayari waliokuwa nao wachezaji wangu,” alisema Mayanja ambaye kikosi chake hivi karibuni kililambwa 2-0 na Yanga katika mchezo wa ligi.
Kocha huyo raia wa Uganda, alisema kinachompa matumaini ni uwajibikaji mzuri wa wachezaji wake mazoezini, lakini pia uelewano waliouonesha katika mchezo dhidi ya Singida United.
Alisema katika mchezo huo wachezaji wake walijituma na kuonesha umakini mkubwa jambo lililomfanya aamini hawana tena mawazo ya kipigo kutoka kwa Yanga na kwamba atahakikisha utulivu na umakini wa vijana wake uwanjani unaendelea hadi katika mchezo dhidi ya Mbeya City na mechi nyingi zinazofuata ili kujipatia ushindi mnono.
Kocha huyo raia wa Uganda alisema katika mchezo huo anafikiria kumwanzisha beki Novaty Lufunga kuziba nafasi ya Hassan Isihaka aliyesimamishwa kwa muda usiojulikana akihusishwa na utovu wa nidhamu.
Simba inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 45, lakini Mayanja amesema bado timu hiyo ina nafasi ya kubwa bingwa msimu huu licha ya kuwa nyuma kwa pointi moja na mchezo mmoja dhidi ya vinara Yanga na Azam.

No comments:

Post a Comment