Wednesday, 9 March 2016

Benki ya Wanawake yakaliwa kooni



Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa siku tatu kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), awasilishe maelezo kwa nini benki hiyo inatoza kiwango kikubwa cha riba kwa wanawake katika mikopo, wakati inapewa fedha na Serikali kwa ajili ya kusaidia kundi hilo.
Pia waziri huyo ametangaza kiama kwa wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya wasiotenga asilimia tano ya bajeti yao kwa ajili ya mfuko wa maendeleo ya wanawake, kuwa kuanzia sasa, watakaoshindwa kutimiza agizo hilo, watatumbuliwa majipu. Alisema hayo jana kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, jijini Dar es Salaam.
Alisema alishitushwa na taarifa aliyopatiwa juzi katika sherehe za kukabidhi mikopo kwa wanawake zilizofanywa na Benki ya Posta Tanzania (TPB), baada ya kubaini kuwa benki hiyo ya wanawake inatoza kiasi kikubwa cha riba katika mikopo yake.
“Nilisikitika sana kusikia eti TPB inatoza vikundi vya akina mama riba ya asilimia 11 wakati benki ya wanawake inatoza riba ya zaidi ya asilimia 19. Hili siwezi kulikubali hivi inaingia akilini kweli wanawake kushangilia benki nyingine wakati ipo benki ya wanawake kwa ajili yao, tena iliyoanzishwa kwa ruzuku ya Serikali? Alihoji.
Alimtaka Mkurugenzi wa benki hiyo, Margareth Chacha (aliyekuwepo kwenye maadhimisho hayo), kumpatia maelezo ndani ya siku tatu kwa nini benki hiyo inatoza kiwango hicho kikubwa cha riba. “Nataka mnieleze kwa nini benki hii si rafiki kwa wanawake wakati inapewa fedha na Serikali.”
Alisema imemuumiza kuona wanawake wa jiji la Dar es Salaam wakiikimbia benki yao iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwakwamua kimaendeleo na kukimbilia benki nyingine. “Nawahakikishia wanawake wenzangu hili ni jipu tutalitumbua.”
Alisema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inawawezesha wanawake kiuchumi na ndio maana ilianzisha benki hiyo ya wanawake, mifuko mbalimbali ya maendeleo ya wanawake, Taasisi za Kuweka na Kikopa (Saccos) na Vikoba.
Katika eneo la mifuko ya maendeleo ya wanawake, Waziri huyo alifafanua kuwa Serikali kwa mujibu wa Sheria ilianzisha mifuko hiyo na kuzitaka halmashauri zote nchini kutenga kiasi cha asilimia tano katika bajeti yake kwa ajili ya mifuko ya maendeleo ya wanawake.
“Nafahamu kwamba katika halmashauri nyingi hili limekuwa halifanyiki. Napenda niweke wazi kuwa hatutashindwa kuwawajibisha wakurugenzi wote wasiotenga kiasi hiki cha fedha kwa ajili ya mfuko wa wanawake.
Kuanzia sasa Mkurugenzi yeyote asiyetenga asilimia tano kwanza ni adui wa wanawake na pili tutampeleka kwa Rais John Magufuli kwa hatua zaidi,” alisisitiza. Aidha alisisitiza kuwa wizara yake itatafuta orodha ya wakurugenzi wote wasiotenga kiasi hicho cha asilimia 50 kwa ajili ya wanawake na kuiwasilisha orodha hiyo kwa Dk Magufuli kwa kuwa si tu wamewadharau wanawake, lakini pia wamedharau agizo la Rais huyo.
Alisema pamoja na jitihada zinazoendelea kufanyika kuwainua wanawake ili kuweza kufikia lengo la 50 kwa 50 kama ilivyo kauli mbiu ya maadhimisho ya wanawake mwaka huu inayosema 50 kwa 50 ifikapo 2030; tuongeze jitihada, bila kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi, lengo hilo haliwezi kutimia ipasavyo.
Alisema kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2010 katika kila Watanzania 100, 23 ni wanawake wenye kipato kinachozidi au sawa na wanaume. “Sasa kwa nini tusiwe wote na kipato sawa 50 kwa 50 hili linawezekana tukitekeleza mipango yetu ipasavyo.”
Akizungumzia mafanikio ya Serikali katika kuhakikisha usawa na haki kwa wanawake, alisema kwa sasa Tanzania imepiga hatua na kiwango cha uwiano kati ya wanaume na wanawake katika ngazi za maamuzi kimepanda ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, aliwataka wanawake kutumia fursa hiyo kutafakari nafasi ya wanawake na mtoto wa kike katika jamii, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanashiriki katika ngazi za maamuzi.

No comments:

Post a Comment