Thursday, 3 March 2016

Kampuni za simu nchini zapigwa faini ya mamilioni


Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoza kampuni tano za simu za mkononi, faini ya Sh milioni 112.5 kutokana na kushindwa kutekeleza masharti na vigezo vya ubora wa huduma
Ingawa haikuelezwa moja kwa moja vigezo vya ubora wa huduma walivyokiuka, TCRA imezungumzia malalamiko ya wateja ya kukatwa fedha na kampuni bila kupiga simu, na kukiri kukithiri kwa tatizo hilo. Ilisema wanatarajia kufunga mtambo utakaokuwa ukifuatilia bando katika simu za wateja, kukabili tatizo husika.
Kampuni zilizoadhibiwa kwa kukiuka Kanuni ya Ubora wa Huduma za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2011, ni Airtel Tanzania Limited, Benson Informatics Limited (Smart), MIC Tanzania Limited (Tigo), Vodacom Tanzania Limited na Zanzibar Telecom Limited (Zantel).

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba alisema TCRA imebaini kampuni hizo hazitoi huduma bora. Ilibaini hilo baada ya kutathmini ubora wa huduma za mawasiliano (Sauti na data) zinazotolewa na kampuni hizo. Tathmini ililenga kupata uhalisia wanaoupata watumiaji wa huduma hizo.

“Kwa kuzingatia makampuni hayo kukubali kutotimiza vigezo vya ubora wa huduma wanazotoa na kuahidi kuboresha, Mamlaka imetoa adhabu kwa mujibu wa kanuni za ubora wa huduma kama ilivyoainishwa katika Kanuni 15 ya Kanuni ya Ubora wa Huduma,” alisema.

Alitaja kampuni na faini (kwa shilingi) wanazotakiwa kulipa ndani ya mwezi mmoja ni Airtel (Sh milioni 22.5), Benson Informatics Limited(Sh milioni 12.5), Tigo (Sh milioni 25), Vodacom (Sh milioni 27.5) na Zantel (Shmilioni 25).

“Endapo makampuni hayo yatashindwa kutoa faini hizo katika muda waliotakiwa kutoa au makosa hayo kujirudia rudia, watachukuliwa hatua kali zaidi, ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni,” alisema.
Dk Simba aliwasisitiza watoa huduma za simu za mikononi, kuhakikisha huduma hizo zinazingatia vigezo vilivyoainishwa kupitia Kanuni za Ubora wa Huduma na kuboresha huduma hizo katika kipindi cha miezi sita. Alisema mamlaka itaendelea kufanya uchunguzi wa ubora wa huduma za simu sehemu mbalimbali nchini, kila baada ya miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment