Wednesday, 2 March 2016

Taifa Stars kuivaa Chad kimtindo




Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa
TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars haitaweka kambi ya maandalizi ya mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za michuano ya Kombe la Mataifa Afrika dhidi ya Chad inayotarajiwa kuchezwa baadaye mwezi huu Dar es Salaam kabla ya kurudiana siku tatu baadaye
Hiyo ni kutokana na mwingiliano wa ratiba ya Ligi Kuu Tanzania bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Hivi karibuni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi alisema kwa sasa hakuna mpango wa kuibadilisha ratiba ya ligi ili kumalizika kwa wakati uliopangwa labda kwa mechi za Yanga na Azam ambazo zinashiriki michuano ya kimataifa.
Akizungumza na gazeti hili jana Kocha Mkuu wa Taifa Stars Charles Mkwasa alithibitisha hilo.
“Ni kweli hatutakuwa na muda, lakini ndivyo mambo yalivyo tutakuwa na muda mdogo wa maandalizi,” alisema.
Baada ya mechi za ligi za mwishoni mwa wiki kwa Yanga na Azam ambazo hutoa wachezaji wengi wa timu ya taifa zitalazimika kujiandaa na michuano ya Afrika ambazo zote zitacheza siku moja Machi 11, mwaka huu Rwanda na Afrika Kusini.
Yanga inatarajia kucheza dhidi ya APR ya Rwanda baada ya kufuzu hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa huku Azam ikicheza mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Bidvest.
Timu hizo zitakaporudi zitacheza mchezo mmoja wa ligi kisha zitaanza maandalizi ya michezo ya marudiano ya kimataifa Machi 19, mwaka huu Dar es Salaam.
Stars inatarajiwa kuondoka Machi 20 kuelekea N’Djamena, Chad kwa ajili ya mchezo wa Machi 23, mwaka huu hivyo, kuna uwezekano kuwakosa wachezaji wengine ambao ni tegemeo kutokana na kutumikia timu zao.
Baada ya mchezo dhidi ya Chad Taifa Stars inatarajiwa kurudi siku inayofuata ili kujiandaa tena kwa siku mbili kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Machi 27, mwaka huu Dar es Salaam.
Mkwasa anatarajia kutangaza kikosi cha Taifa Stars Jumanne ijayo kisha kusubiri wachezaji hao, lakini huenda akapata wakati mgumu kupata kikosi anachokihitaji kutokana na ratiba kubana.

No comments:

Post a Comment