Thursday, 31 March 2016

Marekebisho sheria ya manunuzi kukabidhiwa Mwakyembe leo


Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe.



TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania leo itakabidhi taarifa ya utafiti wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011, Sura ya 410 kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe. Utafiti huo ulifanywa na Tume kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 8(1) na (2) cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria.

Ofisa Habari wa Tume hiyo, Munir Shemweta alisema mbali ya masharti ya kifungu hicho, pia taarifa hiyo ina hadidu za rejea zilizotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo aliitaka Tume kubainisha upungufu katika utekelezaji wa sheria na kubainisha madhara ya upungufu huo katika utekelezaji kwa serikali na taasisi zake.

Shemweta alisema katika utafiti Tume ilikutana na wadau mbalimbali kutoka Wizara, Idara,Taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali wakiwemo watalaamu waliobobea katika masuala ya ununuzi wa umma. Alisema taarifa ya Tume ina mapendekezo ya namna ya kuiboresha sheria hiyo ili ilete tija zaidi katika sekta ya ununuzi wa umma.

Utafiti wa sheria hiyo ulianza hivi karibuni ikiwa ni kuitikia agizo la Rais John Magufuli ambaye aliahidi kuifanyia marekebisho sheria hiyo wakati analizindua Bunge la 11 mwishoni mwa mwaka jana.

Akilihutubia Bunge katika eneo la kuziba mianya ya rushwa, Dk Magufuli aliahidi kuifumua sheria hiyo ambayo inatoa mianya kwa watumishi wa umma kuiba fedha za umma. “Tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu tunaiziba” alisema Rais.

No comments:

Post a Comment