Wednesday, 2 March 2016

Azam ni fainali- Pluijm




Kocha Mkuu wa Yanga, Hans-van-der-Pluijm

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Azam ni sawa na fainali kwao, kwani ushindi utawaweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu.
Timu hizo zinatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga huku zikiwa zinalingana kwa pointi kila moja ikiwa na pointi 46 zilizopatikana katika michezo 19, waliyocheza.
Katika mawasiliano yake na gazeti hili kwa njia ya mtandao akiwa kambini Pemba jana, Pluijm alisema wameupa uzito mkubwa mchezo huo kwa vile wanajua umuhimu wa ushindi hivyo atahakikisha wanaitumia vizuri nafasi hiyo kufanya maandalizi ya kutosha ili washinde.
“Kila mchezaji wangu anajua umuhimu wa ushindi katika mchezo huo na Azam ni moja ya timu ngumu ambayo imekuwa ikitusumbua kila tunapocheza nao, lakini Jumamosi tunataka kudhihirisha kuwa Yanga ni timu kubwa Tanzania,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo alisema wamejipanga kutetea ubingwa wao msimu huu na kuifunga Azam itakuwa imewapa uhakika wa asilimia 95 kutimiza lengo lao ambalo ni ubingwa wanaoushikilia hivi sasa baada ya kufanya hivyo msimu uliopita.
Alisema anawaheshimu Azam kwa kuwa ni moja ya timu inayofanya vizuri kwenye ligi na ambayo imekuwa na upinzani mkubwa kwao lakini amekiandaa kikosi chake kuhakikisha hawafanyi makosa Jumamosi kwa kupata ushindi ambao utawaweka karibu na taji hilo kama ambavyo wamekusudia.
“Tumekuja Pemba kuweka kambi sehemu hii imekuwa na mafanikio kwetu tumevuna pointi sita mbele ya Simba msimu huu kambi yetu ikiwa hapa hivyo tumeona tuje huku wakati tunajiandaa kucheza na Azam huenda bahati ikaendelea kuwa kwetu na kushinda mchezo huo,” alisema Pluijm.
Kocha huyo alisema tayari amewaandalia Azam mfumo mpya watakaoutumia kwa mara ya kwanza akiamini utawasaidia kupata ushindi kirahisi kutokana na namna alivyowasoma na kugundua mapungufu yao .
Mshindi katika mchezo huo atakuwa na nafasi kubwa ya kumtambia mwenziwe, baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, Yanga ikianza kufunga kupitia kwa Donald Ngoma na Azam ikasawazisha kipindi cha pili mfungaji akiwa Kipre Tchetche.

No comments:

Post a Comment