Mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima.
YANGA na Azam kazi leo. Wawakilishi hao wa Tanzania katika
michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF),
leo wanashuka viwanjani ugenini katika mashindano tofauti kusaka pointi.
Yanga itakuwa mgeni wa APR kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali,
Rwanda huku Azam FC pia ikiwa mgeni wa Bidvest Wits kwenye Uwanja wa
Bidvset nchini Afrika Kusini. Yanga, mabingwa wa Tanzania Bara,
watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 3-0 nchini humo
walipokutana kwa mara ya kwanza na APR mwaka 1996.
APR yenye wachezaji wengi wa timu ya Taifa ya Rwanda sio timu ya
kuidharau, kwani iliwahi kuitoa Yanga katika raundi ya kwanza ya
michuano hiyo mwaka huo kwa jumla ya mabao 3-1 ikishinda 3-0 kwao na ule
wa marudiano uliochezwa Dar es Salaam Yanga ikishinda bao 1-0. Timu
hizo zimekuwa zikitambiana kupata ushindi kutokana na jinsi ambavyo kila
mmoja amekuwa akifanya vizuri katika ligi yake.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm kabla ya kuwasili Rwanda, alisema
atawaandaa wachezaji wake kisaikolojia na kimashindano kuhakikisha
wanapata ushindi ugenini ili kutengeneza mazingira mazuri ya mchezo wa
marudiano utakaochezwa baada ya wiki moja. Yanga ilivuka raundi hiyo
baada ya kuitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0.
Wakati huo huo, habari zilizopatikana kutoka Kigali, Rwanda jana
zilisema kuwa kiungo nyota wa Yanga, Haruna Niyonzima amekuwa gumzo
kubwa kuhusu mchezo huo. Niyonzima aliyejiunga na Yanga msimu wa mwaka
2011/12 akitokea APR ya Rwanda anaelezwa kuwa ni mchezaji anayependwa
kuliko wote miongoni mwa mashabiki wa soka wa Kigali, Rwanda, hasa
kuelekea mchezo wa leo.
Kwenye mazoezi ya Yanga yaliyofanyika juzi na jana, mashabiki
walifurika uwanjani na gumzo kubwa likiwa ni Niyonzima. “Amepokelewa kwa
shangwe sana na jana kwenye mazoezi yetu mashabiki walifurika sana
kumuangalia, anapendwa sana hapa Kigali,” alisema Meneja wa Yanga,
Hafidh Saleh.
Mbali na Niyonzima, mashabiki wa APR wamekuwa wakiulizia mara kwa
mara taarifa za wachezaji kama vile Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amis
Tambwe na winga Simoni Msuva wanaowachukulia kama ni hatari kwao
kuelekea mchezo huo.
”Wana taarifa za akina Ngoma, Tambwe, Kamusoko na Msuva ambao kwao
wanawachukulia ni hatari sana kuelekea mechi hiyo, mazungumzo na maswali
yao ni juu ya hawa jamaa, wameanza kuingiwa hofu hasa wakisikia habari
juu ya viwango vyao,” alisema Saleh.
Saleh alisema kwamba wachezaji wote wako kwenye hali nzuri kuelekea
mchezo huo isipokuwa kiungo Saidi Makapu anayesumbuliwa kifua na mafua.
Wakati huo huo, akizungumzia mchezo huo Niyonzima alisema ana imani leo
Yanga itaibuka na ushindi mnono.
“Anayekwambia mchezaji ana mapenzi na timu, huyo anakudanganya,
nilicheza APR lakini kwa sasa nipo Yanga na ndipo kazini kwangu, siwezi
kucheza kwa mapenzi kwenye mechi hiyo eti kwa sababu nilikuwa APR,
nitaonesha uwezo wangu wote na nikipata nafasi ya kuwafunga
nitawafunga,” alisema Niyonzima.
Hata hivyo, aliwaonya wachezaji wenzake kujituma kwani japo APR
inaundwa na wachezaji wengi chipukizi kwa sasa ni timu nzuri inayoweza
kufanya chochote kwenye mechi yoyote na hivyo haitakuwa mechi rahisi.
Kwa upande wa Azam FC wanakutana na Bidvest kwa mara ya kwanza, hivyo
ni timu zisizofahamiana, lakini kila moja huenda ikacheza kwa tahadhari
kutokana na kusomana mapema.
Wakati Azam FC ikianzia raundi hiyo ya kwanza, Bidvest Wits imefika
hatua hiyo baada ya kuiondosha Light Stars ya Shelisheli kwa mabao 9-0,
ikianza kwa kushinda ugenini 3-0 kabla ya kuichapa tena 6-0 nyumbani.
Kocha Msaidizi wa Azam, FC Mario Marinica, alisema wameiona Bidvest Wits
kwenye mechi kadhaa na wanajua mbinu wanazotumia na kwamba wanayo
nafasi nzuri ya kuwatoa Wasauzi hao.
“Tunauchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa, hata wapinzani wetu nao
tunawachukulia kwa uzito mkubwa, tayari tumeshawapeleleza kwenye mechi
kadhaa, tunajua ubora wao na ni timu nzuri, ila sisi tuko kamili na
tayari kucheza nao,” alisema.
Naye mshambuliaji wa Azam FC, Allan Wanga amesema kuwa anaweza
kuifunga Bidvest Wits ya Afrika Kusini, endapo atapewa nafasi ya kucheza
leo. Kwa mujibu wa tovuti ya Azam, Wanga anajipa matumaini hayo
kutokana na kuijua vema Bidvest Wits baada ya kufanya majaribio ya wiki
mbili Juni mwaka jana, kabla ya kutua Azam FC.
“Nilikuwa mwezi wa sita mwaka jana hapa Bidvest Wits nikafanya vizuri
kwa wiki mbili kwa sababu walitaka kunisaini nikiwa El Merreikh tangu
miaka miwili iliyopita baada ya mazoezi ikawa wamekubaliana na wakala
wangu ili kunisajili, lakini wakati huo mama yangu (marehemu) alikuwa
amezidiwa na ugonjwa na kibali changu cha kazi hapa kilikuwa
hakijatoka,” alisema.
Nyota huyo wa kimataifa kutoka Kenya, alizungumzia aina ya soka
wanalocheza Bidvest Wits na kudai kuwa timu hiyo haichezi soka la pasi
kama zilivyo timu nyingine huko Afrika Kusini bali hucheza zaidi mipira
mirefu.