Tuesday, 23 February 2016

Yanga yanoa makali




Kikosi cha Yanga

BAADA ya kuinyoosha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwishoni mwa wiki, Yanga leo inaingia kambini kujiandaa na mechi mbili, imeelezwa
Kesho Jumatano, Yanga ambao ni mabingwa wa Tanzania Bara, watacheza na JKT Mlale katika mchezo wa Kombe la FA kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku Jumamosi wakiwa na kibarua dhidi ya timu ya Mauritius ya Cercle de Joachim.
Katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika uliopigwa Mauritius mwishoni mwa wiki iliyopita, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na hivyo kuhitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili kusonga mbele.
Yanga inacheza mechi hizo mbili ikiwa iko vizuri baada ya Jumamosi kuwafunga watani zao wa jadi Simba kwa kuwafunga mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulioirejesha timu hiyo kileleni mwa msimamo wa ligi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema kikosi hicho kitaweka kambi yake jijini.
“Tunashukuru Mungu tulimaliza mchezo wetu na Simba salama kwa kupata ushindi mzuri, kikosi kimeanza mazoezi leo (jana) kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini na kesho(leo) kitaingia kambini kujiandaa na michezo ijayo,” alisema.
Muro alisema wamejiandaa kufanya vizuri katika mchezo huo ili kutimiza malengo waliyojiwekea ya kufika hatua ya makundi. Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umewapongeza wachezaji na benchi nzima la ufundi kwa kufanya vizuri katika mchezo uliopita dhidi ya Simba na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
“Uongozi wa Yanga unawapongeza wachezaji na kuwashukuru benchi la ufundi kwa kufanya kazi nzuri ile waliyotumwa, ni kazi waliyopewa na taifa la Watanzania, lakini pia tunawapongeza wanachama, mashabiki na wapenzi waliounga mkono timu,” alisema.
Muro alisema kwenye suala la Ligi Kuu wamefunga ukurasa na watani wao Simba na kwamba sasa sio wapinzani wao bali wamebaki kuwa watani wao wa jadi.

No comments:

Post a Comment