ZAIDI ya askari 200 kusimamia mbio za 14 za Kilimanjaro Marathoni zitakazofanyika kesho mjini Moshi, imebainishwa.
Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAA), Amini Kimaro alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili kuhusu maandalizi ya mwisho kuhusu mbio hizo.
Kimaro alisema mbali na askari polisi ambao watalinda usalama katika maeneo mbalimbali zitakapofanyikia mbio hizo, pia kutakuwa na wasimamizi wengi ili kuhakikisha washiriki hawakatishi njia.
Kumekuwa na malalamiko mengi kuwa baadhi ya wanariadha wanaoshiriki mbio hizo kukatisha njia ili kupata ushindi. Alisema mwaka huu kila baada ya kilomita tano mbali na kuwa na vituo vya maji, pia kutakuwa na waangalizi ambao watakuwa wakirekodi namba za wakimbiaji ili wasikatishe njia.
Kimaro alisema kuwa pia kutakuwa na vifaa maalumu vya kielektroniki kufuatilia mwenendo mzima wa washiriki na kuhakikisha hakuna anayejaribu kukatisha njia.
Alisema kuwa kutakuwa pia na magari ya kuongoza mbio hizo pamoja na magari ya wagonjwa yatakayokuwa nyuma ya wakimbiaji wa mbio mbalimbali.
Alisema mbio za kilomita 42 zitaanza saa 6:30 huku zile za nusu marathoni za Tigo zitaanza saa 12:45 asubuhi wakati za kilomita 10 za walemavu zitaanza kutimua vumbi saa 1:00 asubuhi. Alisema mbio za kujifurahisha za kilomita tano zenyewe zinataraja kuanza saa 1:30 asubuhi.
No comments:
Post a Comment