Saturday, 27 February 2016

Cheka mtihani mgumu leo



NANI kugeuka kitoweo kati ya Francis Cheka na Geard Ajetovic?
Leo litapigwa pambano la kimataifa la ubingwa wa mabara kwenye viwanja va Leaders, Dar es Salaam huku mabondia wote wawili wakitambiana kumalizana.
Mabondia hao wanapigania uzito wa kilo 72 ubingwa wa mabara, ikiwa ni mara ya pili kukutana baada ya mwaka 2008 kukutana kule Manchester nchini Uingereza ambapo Cheka alipigwa kwa pointi.
Cheka alisema jana kuwa hatawaangusha Watanzania kwani amejipanga kumgeuza Ajetovic kitoweo.
“Naahidi kwamba mkanda huu wa dunia utabaki nyumbani, sitawaangusha Watanzania, watu waje kwa wingi kushuhudia watajua nani kuwa bingwa,” alisema.
Bondia huyo wa Tanzania alizungumza kwa maneno ya kimakonde kutamba kuwa kilichoumbwa na Mungu sio haramu kuliwa, hivyo, ni halali yake kummaliza bondia huyo wa Uingereza mapema na kuwa kitoweo chake.
Kwa upande wa Ajetovic alisema atammaliza Cheka kwa KnockOut (KO) raundi ya nne tu na kuuchukua mkanda huo.
Alisema amejipanga kushinda hivyo hana wasiwasi huku akimwita Cheka kuwa ni babu hana lolote. Pambano hilo la kimataifa litasindikizwa na burudani kutoka bendi ya Twanga Pepeta.

No comments:

Post a Comment