Jitihada za kumpata Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuzungumzia suala hili hazikuzaa matunda kwani yupo safarini kikazi ambapo msaidizi wa waziri huyo alimwambia mwandishi awasiliane na Katibu Mkuu, kwa ufafanuzi zaidi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu alijibu kupitia ujumbe mfupi wa maneno (sms) kuwa anaongoza kikao cha wadau wa usafirishaji, atarudi ofisini saa moja jioni.
Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen Ngatunga alisema jana wakati wa Mkutano Mkuu wa wadau wa Taffa uliofanyika Dar es Salaam kuwa serikali ilisikia kilio chao cha kutaka tume huru ya kuchunguza uozo uliopo bandarini ambao umesababisha wanachama wao kutozwa malipo mara mbili.
“Baada ya kilio chetu cha muda mrefu kuhusiana na yale yalipo hivi sasa baina ya kampuni za wakala za forodha na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuwa watu wa forodha ni wezi, sasa serikali imeamua kuunda tume maalum ambayo inaanza kazi kesho (leo) na hapo ndipo ukweli utakapobainika kati yetu na hao watu wa TPA,” alieleza Ngatunga.
Alisema kumekuwapo na mianya ya wizi wa fedha nyingi unaofanyika kati ya TPA na benki zilizopewa idhini ya kukusanya ushuru wa forodha bandarini, jambo linalosababisha kampuni zao kutuhumiwa kukwepa kodi na wizi.
Alisema kampuni nyingi ziliwasilisha vielelezo vyao juu ya malipo yote waliofanya, lakini bado walitakiwa kulipa tena ikielezwa kuwa stakabadhi walizotoa hazikuwa halali, lakini hundi walizolipa hazikukataliwa.
Aidha, alidai viongozi wa TPA wamempa taarifa za uongo Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na matokeo yake ni kutumbuliwa majipu kwa watu wa chini, lakini tatizo kubwa bado lipo pale pale bandarini hapo.
“Tunamuomba Rais atupie upya macho TPA kwani watu walioondolewa ni vidagaa tu, lakini mapapa bado wapo na tatizo bado lipo pale pale. Kuachwa kwa watu hao kunafanya kampuni za forodha za kimataifa zilipo hapa nchini kuhamishia shughuli zao bandari za nchi jirani,” alidai Ngatunga.
Ngatunga alisena ni ngumu kuamini kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, mawakala wa forodha wakawa wanakwepa tu kulipa ushuru na viongozi wa bandari wapo.
Mwakilishi wa Kampuni ya Freight Fowarder Tanzania (FFT), Leonard Mwakikao alidai kampuni yake iliamriwa kulipa kiasi cha Sh milioni 41 ambazo baada ya kufuatilia malipo hayo iliyofanya mwaka 2013, ilibainika kuwa hundi yake ya malipo ililipia mizigo ya kampuni nyingine na si ya kwao kama ilivyoagiza.
No comments:
Post a Comment