Monday, 29 February 2016

Kuna mbinu mpya za kusafirisha mirungi




Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Mihayo Msikhela

POLISI mkoani Tanga imesema imegundua mbinu mpya ya usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi kwa kuziweka kwenye madumu tupu yaliyokuwa na mafuta.
Mbinu hiyo inadaiwa kutumiwa na baadhi ya wasafirishaji wa dawa hizo kuziingiza mkoani humo wakikwepa kukamatwa na askari kwenye vizuizi barabarani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Mihayo Msikhela aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kwamba wasafirishaji hao hujaza mirungi ndani ya madumu matupu ya ujazo wa lita 20 yaliyokuwa na mafuta ya kupikia na kisha kuyasafirisha katika magari mbalimbali ya mizigo.
Alisema wamebaini mbinu hiyo kutokana na jitihada za askari waliokuwa doria katika kizuizi cha polisi kilichopo eneo la Amboni kati ya saa 10 hadi 11 jioni baada ya kukamata lori namba T 342 CVY aina ya Nissan lililokuwa likisafirisha mchanga kwa ajili ya ujenzi kutoka kijiji cha Mpirani kwenda jijini Tanga.
“Jana jioni askari waliokuwa doria nje ya mji eneo la Mpirani lililopo kata ya Chongoleani walikamata watu saba waliokuwa wakisafirisha kilo 73 za mirungi kwa kutumia lori la mchanga kwa kuweka dawa hizo ndani ya madumu yaliyokuwa yametumika kuhifadhia mafuta ya kula na kisha kuyafunika na kifusi cha mchanga kilichokuwa ndani ya lori hilo”, alisema.
Aliongeza, “Baada ya kujaza mirungi madumu hayo waliyafukia ndani ya shehena ya mchanga uliokuwa unasafirishwa kwenda eneo la Kwanjeka jijini Tanga kuuzwa kwa mteja”, alisema.
Kamanda Mihayo aliwataja watuhumiwa wanane waliokuwa wakisafirisha mirungi hiyo ambao wote ni wakazi wa mkoani hapa, akiwemo dereva wa lori.
Alisema wote watafikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment