Thursday, 18 February 2016

Tanzania yapongezwa kwa kutojitoa ICC


Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Dk Steven

SERIKALI imepongezwa kwa busara na msimamo wake wa kutojitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), kwani kuwepo kwa mahakama hiyo kunasaidia kupata haki kwa wanyonge.
Imeelezwa kuwa Umoja wa Afrika (AU) unafanya kosa kubwa kuhamasisha wanachama wake kujitoa katika mahakama hiyo na kutaka Tanzania kutofuata mkumbo.
Pongezi hizo zilitolewa jana na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Dk Steven Bwana ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) nchini Cambodia, alipozungumza na gazeti hili.
Jaji Bwana alisema faida ya kuendelea kuwepo kwenye mahakama hiyo ni amani ya kitaifa kuendelea kuwepo kwani ICC ipo kwa ajili ya kutafuta haki za wanyonge kutoka kwa viongozi wanaojifanya miungu watu.
“ICC inakuwa na nguvu ya kukamata viongozi kwa nia njema kwani kuna baadhi ya viongozi au watu ukiwahukumu katika mahakama za nchini wanaweza kusababisha haki isitendeke kwani wapo wenye nguvu ya kuingilia maamuzi ya mahakama nchini mwao,” alifafanua Jaji Bwana.
Jaji Bwana alisema hivyo ICC husimamia kesi kimataifa kwa kuwa na nguvu ya kuwakamata watu hao wanaojifanya miungu watu katika nchi zao ili haki itendeke.
Alitaka AU kuangalia maamuzi wanayotaka yana madhara gani kwani kuhitaji kiongozi kushtakiwa baada ya kustaafu inaweza kusababisha haki isitendeke kwa mashahidi kuhongwa na kupindisha ushahidi au kwa viongozi wanaokaa miaka 20 hadi 30 ni vigumu mashahidi kuwapata kirahisi.
Juzi serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga ilisema haitajitoa katika mahakama hiyo ya ICC, lakini walitaka tabia ya ubaguzi dhidi ya viongozi wa Bara la Afrika inayooneshwa na mahakama hiyo inaweza kurekebishwa.

No comments:

Post a Comment