Sunday, 28 February 2016

Ufisadi wa vitabu waathiri darasa la kwanza



Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Teknolojia, Sayansi na Ufundi, Maimuna Tarishi akitoa tamko la Serikali la kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) baada ya kushindwa kutekeleza maagizo ya kusitisha uchapaji wa vitabu vya kiada kwa darasa la kwanza ambavyo vilikuwa na kasoro. Mwingine ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Leonard Akwilapo. (Picha na Fadhili Akida).

UFISADI uliofanyika katika uchapaji wa vitabu 2,807,600, vilivyo tayari kutumika kwa ajili ya darasa la kwanza nchi nzima, umesababisha wanafunzi hao, ambao mwaka huu udahili wao umeweka historia kwa idadi kubwa kuwahi kudahiliwa, kulazimika kutumia vitabu vya zamani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna Tarishi (pichani), alisema hayo jana alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam. Alifafanua kwamba kasoro kubwa, zilizobainika katika vitabu hivyo, ambavyo vilishafika katika ghala la Serikali, zimesababisha Serikali izuie visisambazwe.
Kwa mujibu wa Tarishi, vitabu hivyo vya ‘Najifunza Kusoma Kitabu cha Kwanza’ na ‘Najifunza Kusoma Kitabu cha Pili’, vimechapwa na kampuni ya Yukos Enterprises, ambayo ni moja ya kampuni tatu zilizoshinda zabuni ya kazi hiyo iliyotangazwa Aprili mwaka jana.
Lakini, alisema kasoro hizo zimesababisha Serikali kuagiza viondolewe katika ghala lake na udhibiti ufanyike visisambazwe mashuleni.
Upungufu
Kasoro zilizokutwa ni muingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa, picha moja kuwa na rangi tofauti, ukataji usiozingatia vipimo, baadhi ya vitabu kufungwa kwa pini moja katikati badala ya mbili, huku vingine vikikosa pini kabisa na vingine vikifungwa ubavuni.
Kasoro nyingine ni vingine vimekutwa vimechakaa kabla ya matumizi, hasa kitabu cha ‘Najifunza Kusoma Darasa la Kwanza Kitabu cha Pili’; vingine vikiwa na mpangilio mbaya wa kurasa, ufifiaji wa maandishi huku picha katika baadhi ya vitabu na maandishi, vikishindwa kuonekana kabisa.
Kasoro nyingine kwa mujibu wa Tarishi ni namba za kurasa kutoonekana kabisa, baadhi ya kurasa kujirudiarudia, baadhi ya kurasa kutotenganishwa, maandishi ya baadhi ya vitabu kugeuzwa mwelekeo, majalada kuwa zaidi ya moja na baadhi ya vitabu kukutwa vimedurufiwa (photocopy).
Katibu Mkuu huyo alisema kasoro hizo, zilibainika baada ya ufuatiliaji kufanywa na Wizara katika bohari iliyokuwa ikipokea vitabu hivyo.
“Kutokana na kasoro hizo, ni dhahiri mchapaji Yukos Enterprises Ltd hakuzingatia vigezo vilivyowekwa na kwa kufanya hivyo amekiuka makubaliano yaliyo katika mkataba alioingia na Taasisi ya Elimu Tanzania,” alisema Tarishi.
Athari zake
Kutokana na hali hiyo, Tarishi alisema wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka huu watapungukiwa vitabu vya kujifunza kusoma, kwa kuwa haviwezi kutumika. Hivyo aliagiza wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka huu, watumie vitabu vya zamani na walimu watatumia ‘Kitabu cha Kiongozi cha Mwalimu’ ambacho ni kipya.
Kuhusu gharama iliyotumika, Tarishi alisema ni zaidi ya Sh bilioni mbili, lakini alibainisha kuwa mchapishaji alikuwa amelipwa asilimia 20 tu kwa kutumia dhamana ya benki.
Majipu yatumbuliwa
Kasoro hizo zimemlazimu Katibu Mkuu huyo kuagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), kuwasimamisha kazi vigogo wa taasisi hiyo, akiwemo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Vifaa vya Kielimu, Peter Bandio, Mwanasheria, Pili Magongo na Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Jackson Mwaigonela.
Hatua hiyo imetakiwa kufuatia uchunguzi katika taasisi hiyo, kuhusu vipi wameshindwa kusimamia Sheria ya Manunuzi na kazi ya uchapaji wa vitabu.

No comments:

Post a Comment