Saturday, 27 February 2016

Ajali yaua wanne


WATU wanne wamekufa akiwamo daktari wa wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro, Albion Kasasa huku abiria wanane wakijeruhiwa kwa kukatika viungo mbalimbali vya miili yao baada ya basi dogo na gari kugongana katika barabara kuu ya kutoka Shinyanga maeneo ya Maganzo kwenda jijini Mwanza.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 10:30 jioni katika Kijiji cha Buganika, kata ya Songwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo basi dogo lenye namba za usajili T260 DDY aina ya Fuso, mali ya kampuni ya Mashimba ikitokea Kahama kwenda Mwanza kugongana na gari T281 CLJ Honda Station Wagon.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Mika Nyange alisema gari hilo dogo lilikuwa likiendeshwa na daktari kutoka Ifakara, Kasasa ambaye alikufa papo hapo huku majeruhi wakikimbizwa katika hospitali ya rufani mkoani Shinyanga.
Kamanda Nyange alitaja watu wengine waliokufa kuwa ni Ismail Hassani na Subira Elius wote wakazi wa Kahama na Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, Pius Emmanuel wakati majeruhi wanane ni Ramadhani Athumani, Amina Ally, Mwamvua Deo na Anastazia John.
Wengine ni Mrashi Abdalah, Juma Hamza, Ibada Lwegoshola na Ndalawa Mashigani. Kamanda Nyange alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa magari yote mawili .
Naye mmoja wa majeruhi hao Ramadhani Athumani alisema walikuwa wakitokea Kahama kwenda Mwanza na walipofika katika kijiji hicho cha Buganika, ghafla waliona gari dogo likiyumba.

No comments:

Post a Comment