Saturday, 27 February 2016

Mawaziri ‘waliombip’ Magufuli hadharani

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

MAWAZIRI watano wamewekwa hadharani kuwa ndio hawakujaza Tamko la Rasilimali na Madeni na Hati ya Ahadi ya Uadilifu na kurejesha fomu hizo katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana asubuhi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Rais John Magufuli, aliagiza mawaziri hao watekeleze wajibu huo kabla ya saa 12.00 jioni, vinginevyo watakuwa wamejiondoa wenyewe katika nafasi zao.
“Rais ameelekeza mawaziri popote walipo warudi na kutekeleza hilo na ofisi yangu itasimamia kwa karibu kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni na Hati ya Ahadi ya Uadilifu. “Wafanye hivyo na kuzirejesha kabla saa 12 jioni na Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili, atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Majaliwa alisema Rais ameelekeza mawaziri hao watajwe ili popote walipo wajue na kurejea kuzijaza fomu hizo.
Kutokana na maelekezo hayo, Majaliwa aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, ambao hawajarudisha fomu zote mbili za Tamko la Rasilimali na Madeni na Hati ya Ahadi ya Uadilifu.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga ambaye alikuwa hajarejesha Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi wa umma na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ambaye alikuwa hajarudisha Tamko la Rasilimali na Madeni.
Waziri Mkuu alisema Naibu Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira), Luhaga Mpina, yeye alikuwa hajarejesha fomu zote mbili za Tamko la Rasilimali na Madeni na Hati ya Ahadi ya Uadilifu.
Aliweka msisitizao kuwa kiongozi yeyote wa umma, anatakiwa kujaza fomu ya kutamka mali na madeni kwa viongozi wa umma na kuhaidi uadilifu uliotukuka na sheria hiyo itaendelea kufanyiwa kazi kwa wote wanoendelea kuteuliwa.
Akizungumzia suala la mawaziri waliokuwa safari ambao pengine wangeshindwa kuwasilisha fomu hizo, Majaliwa alisema cha muhimu agizo limetolewa na sababu nyingine zitaangaliwa kama zina msingi.
Alisema kama mawaziri hao wako nje ya nchi, ni lazima Rais anajua kwani ndiye anayetoa kibali na ikiwa wako mikoani ambako hawataweza kufika mpaka jana jioni, Waziri Mkuu anafahamu hivyo wataangalia sababu hizo.
Waziri Mkuu amesema wakati akifungua mafunzo ya mawaziri na naibu mawaziri kuhusu Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu yaliyofanyika Ikulu juzi, alikabidhiwa majina ya mawaziri hao.
Akifafanua Majaliwa alisema kila kiongozi anawajibika kutoa tamko la mali na madeni ndani ya siku 30 baada ya kuteuliwa, mwisho wa kutumia wadhifa husika na kila mwisho wa mwaka.
Alisema mawaziri walikabidhiwa fomu hizo walipoteuliwa na viongozi wengine wameendelea kujazafomu hizo na kurudisha kwa Kamishna.
Akizungumza juzi katika mafunzo hayo, Kamishna wa Maadili Jaji mstaafu Salome Kaganda, alisema ofisi yake ilikuwa imepokea fomu za matamko ya mali kutoka kwa baadhi ya mawaziri na baadhi yao walikuwa hawajajaza fomu hizo wala za ahadi ya uadilifu.
Alisema Sheria ya Maadili inamtaka kila kiongozi, kuwajibika kuwasilisha tamko la mali kwa sekretarieti hiyo na jukumu la chombo hicho cha kusimamia maadili ya viongozi, ni kupokea fomu za tamko la kiongozi wa umma za rasilimali, maslahi na madeni.
Jukumu linguine alitaja kuwa ni kupokea, kuchambua na kuchunguza malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukiukwaji wa maadili unaodaiwa kufanywa na viongozi wa umma na kuandaa na kutunza daftari la rasilimali, maslahi na madeni ya viongozi hao.
Alisema sekretarieti hiyo ina wajibu wa kuratibu vikao vya Baraza la Maadili kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma na kuwasilisha kwa Rais taarifa hizo za uchunguzi.
Kwa mujibu wa jaji Kaganda, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, inatamka maadili yanayotakiwa kuzingatiwa na kila kiongozi kuwa ni uadilifu, haki na uwajibikaji ambazo ni sifa muhimu za kiongozi bora.
Jaji Kaganda alisema kwa kuzingatia misingi na miongozo hiyo, katika sheria hiyo mawaziri na wakuu wa mikoa wamewekewa kifungu maalumu kinachobainisha maadili wanayopaswa kuyatekeleza.

No comments:

Post a Comment