Katika Jimbo la Kigoma Kusini, kesi hiyo imeshindwa kusikilizwa jana kutokana na sababu za kisheria na imepangwa Machi 9 mwaka huu.
Aidha katika Jimbo la Longido, kesi ilikuwa ianze jana, lakini iliahirishwa hadi keshokutwa kumpa Jaji husika nafasi kupitia jalada. Kesi katika Jimbo la Nyamagana, imepangwa kuanza kusikilizwa Februari 29 mwaka huu.
Jimbo la Longido
Jana, kesi hiyo katika Jimbo la Longido iliahirishwa kwa siku tatu baada ya Jaji Mfawidhi Kanda ya Bukoba, Sivangilwa Mwangesi aliyepangiwa kuisikiliza, kutaka muda apitie jalada la kesi kufahamu hoja za msingi katika kesi hiyo ya kwanza ya uchaguzi mkoani Arusha.
Jaji Mwangesi alisema hayo mbele ya Mahakama hiyo na kueleza kuwa ameingia jijini Arusha juzi jioni, hivyo hajui kilichomo ndani ya jalada hilo. Aliomba mawakili wampe siku tatu, kulisoma na kujiridhisha kilichomo ndani na keshokutwa atoe mwongozo wa kesi hiyo.
“Ninawaomba mawakili wote mnipe siku tatu kulipitia jalada hili kubwa mno ili niweze kulisoma na kujua kilichomo na Alhamisi wiki hii nitatoa namna ya kuendesha kesi hii mpaka imalizike kwani niko hapa kwa ajili ya kesi hii tu ya uchaguzi,” alisema Jaji Mwangesi.
Kutokana na ombi hilo, mawakili wote walikubaliana na hoja ya Jaji Mwangesi ya kukutana keshokutwa kufahamu mwongozo wa uendeshaji wa kesi hiyo. Ilielezwa pia kuwa huenda kesi hiyo ikasikilizwa mfululizo kuanzia Februari 29 hadi itakapomalizika.
Mawakili wa aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Dk Stephen Kiruswa, wametoa sababu 10 za kutaka matokeo ya uchaguzi huo yatenguliwe. Mawakili hao ni Dk Masumbuko Lamwai, Edmund Ngemera na Daudi Haraka.
Ilidaiwa kuwa miongoni mwa sababu ni kwamba baadhi ya watu waliopiga kura katika jimbo hilo na kumchagua Onesmo Ole Nangole (Chadema), walitoka nchi jirani ya Kenya.
Wakili
Haraka alidai sababu nyingine ni pamoja na masanduku ya kura kubebwa na magari ya wafuasi wa Chadema na kura kutojumlishwa vizuri . Wanadai siku ya kuhesabu kura, wagombea wote walitolewa, lakini mgombea wa Chadema alibaki ndani ya chumba cha kuhesabu kura.
Sababu nyingine ni pamoja na wafuasi wa Chadema na mgombea wao, kufanya siku ya kupiga kura wakati wakifahamu wazi kuwa ni kinyume na utaratibu wa uchaguzi nchini . Inadaiwa mgombea wa Chadema, alitumia lugha isiyokuwa na staha kipindi cha kampeni, ikiwemo matusi na kumdhalilisha mgombea wa CCM.
Kutokana na sababu hizo, mawakili hao walimwomba Jaji kutengua ubunge wa Nangole, kwa kuwa mgombea huyo aliyetangazwa kuwa mshindi wa jimbo hilo, alikiuka taratibu zote za uchaguzi. Katika kesi hiyo, mjibu maombi wa kwanza, Nangole anatetewa na mawakili wawili, ambao ni Method Kimomogolo na Faustin Materu .
Mjibu maombi namba mbili ni msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Longido na wa tatu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanaowakilishwa na Wakili Mfawidhi Arusha, Juma Ramadhani na Fortunatus Mhalila.
Jimboni Nyamagana
Katika Jimbo la Nyamagana, kesi hiyo iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Ezekia Wenje dhidi ya Stanslaus Mabula wa CCM, aliyetangazwa mshindi. Kesi imepangwa kusikilizwa kuanzia Februari 29 mwaka huu.
Akizungumza jana na mawakili wa pande mbili na wananchi waliokwenda mahakamani, kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Robert Makaramba alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa kuanzia Februari 29.
Alisema jaji atakayesikiliza kesi hiyo, amepangwa na Jaji Kiongozi na kesi hiyo itasikilizwa mfululizo. “Mimi siyo Jaji niliyepangiwa kusikiliza kesi hii, Jaji aliyepangiwa anatarajiwa kuwasili leo (jana) jioni hapa jijini Mwanza, haina haja ya kumjua kwa sasa”, alisema Jaji Makaramba.
Alisema Serikali imepanga majaji kusikiliza kesi hizo za uchaguzi kwa uharaka zimalizike kwa wakati. Alisema jaji huyo atakapowasili jijini Mwanza, atakutana na mawakili wa pande zote kupanga utaratibu wa kusikiliza kesi hizo.
“Jaji Kiongozi ndiye aliyemteua jaji wa kusikiliza kesi hii, na mara baada ya kuwasili atakutana na mawakili wa pande zote mbili ili wapange namna ya kusikiliza kesi hizi kwa haraka,” alisema Jaji Makaramba.
Aliwataka mawakili hao kuangalia ratiba za utendaji kazi wao kwa kile alichosema, kesi hiyo itakapoanza itakuwa na vikao vya mfululizo hadi kufikia uamuzi wa kutolewa kwa hukumu.
Katika kesi hiyo, Wenje anatetewa na mawakili wawili; Deya Outa na Elias Hezron huku Mabula akitetewa na mawakili wawili, ambao ni Constantino Mtalemwa na Faustine Malongo.
Serikali katika kesi hiyo, inawakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Bilishanga. Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi, ilifunguliwa na Wenje akipinga ushindi wa Mabula kwa madai kuwa uchaguzi huo haukuwa wa huru na haki. Wenje anadai alipokonywa ushindi wake katika uchaguzi huo.
Jimbo la Kigoma
Kusini Ilielezwa kuwa, kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi Namba 2 ya mwaka 2015, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya NCCR –Mageuzi, David Kafulila katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, ilishindwa kuanza kusikilizwa kutokana na sababu za kisheria. Imeahirishwa hadi Machi 9 mwaka huu.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Kigoma, Silvestre Kainda, alisema kuwa kuahirishwa kuanza kusikilizwa kwa kesi kunatokana na pande zote mbili kukubaliana kurekebisha dosari za kisheria zilizojitokeza.
Kainda alitaka wananchi watulie na kesi itasikilizwa tarehe hiyo kama ilivyopangwa.
Akizungumza kuhusu kuahirishwa kwa kesi hiyo, Profesa Abdallah Safari ambaye ni Wakili wa Kafulila, alidai kumetokana na kutofika mahakamani kwa wadau muhimu ambao kisheria wanapasa kuwepo mahakamani.
Aliwataja walioshindwa kufika mahakamani ni Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili wa Msimamizi wa Uchaguzi na Wakili wa mlalamikiwa, Kennedy Fungamtama ambao kisheria wanapaswa wawepo mahakamani wakati shauri hilo likianza kusikilizwa.
Kwa upande wake, Kafulila alisema kuwa kuahirishwa kwa kesi hiyo kunarudisha nyuma maagizo ya Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi ya kutaka kesi hizo za uchaguzi , zisikilizwe haraka na kumalizika katika muda mfupi
No comments:
Post a Comment