RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa mabalozi, makamishna wanne wa Jeshi la Polisi na pia amemteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, imewataja mabalozi walioteuliwa ni Dk Asha-Rose Migiro, Mathias Chikawe na Dk Ramadhan Dau.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vituo vya uwakilishi kwa mabalozi hawa vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.
Dk Migiro ambaye alikuwa miongoni mwa wana CCM waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais, amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Vile vile amewahi kuongoza wizara mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje; Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria aliyomaliza nayo kwenye Serikali ya Awamu ya Nne.
Kwa upande wake, Chikawe kwa nyakati tofauti aliongoza Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Rais Jakaya Kikwete. Dk Dau aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kabla ya kustaafu.
Kwa upande wa Makamishna wa Polisi, Balozi Sefue aliwataja walioteuliwa ni Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi.
Ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna mstaafu, Suleiman Kova. Mwingine aliyeteuliwa ni Naibu Kamishna wa Polisi, Albert Nyamuhanga ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi.
Ameteuliwa kuongoza Idara ya Fedha, Utawala na Lojistiki, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi, Clodwing Mtweve aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza. Aidha, Naibu Kamishna wa Polisi, Robert Mikomangwa amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Intelijensia.
Kamishna Mikomangwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Valentino Mlowola, aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Nsato Marijani Mssanzya, ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi, ameteuliwa kuongoza Idara ya Mafunzo na Operesheni.
Mssanzya anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi, Paul Chagonja aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.
Pia Rais Magufuli amemteua Dk Modestus Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nida.
Kabla ya uteuzi huu, Dk Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Udhibiti katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Dickson Maimu, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. Uteuzi wote ulianza jana.
No comments:
Post a Comment