Monday, 29 February 2016

Rais awasili Arusha tayari kwa mkutano EAC

Rais John Magufuli akisalimiana na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliyekuwa mmoja wa viongozi na wananchi waliojitokeza kwa wingi kumpokea alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kuongoza mkutano wa 17 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha. (Picha na Ikulu).

RAIS John Magufuli amewasili mkoani Arusha ambako pamoja na mambo mengine ataongoza Mkutano wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika keshokutwa mjini hapa.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Rais Magufuli alilakiwa na viongozi wa serikali, vyama vya siasa pamoja na vikundi vya burudani za ngoma kabla ya kuelekea Arusha Mjini.
Rais Magufuli ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Kabla ya kuongoza kikao hicho, Rais Magufuli anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alhamisi wiki hii, Magufuli na Rais wa Kenya, wataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha - Holili - Taveta - Voi inayounganisha Tanzania na Kenya.
Barabara hiyo ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayotekelezwa na nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment