Mwenyekiti wa Chama cha Mtandao wa Simu Nchini (TEWUTA), Pius Makuke alisema jana kuwa njia hiyo ndiyo pekee itakayoliokoa shirika hilo lisife.
Alisema kwa sasa taasisi nyingi za Serikali zinatumia mashirika binafsi hata kusafirisha vifurushi na barua na kuomba hatua alizochukua Rais Magufuli za kuzuia sukari kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani, pia atumie mbinu hiyo kuzilazimisha taasisi za Serikali kutumia huduma za Posta ili lipate mtaji wa kutosha liweze kujiendesha kwa faida.
Alisema wanatoa ombi hilo kwa Rais kwani baada ya Shirika la Posta kuanzishwa mwaka 1994, Serikali iliahidi kulipatia mtaji, lakini hata hivyo mtaji huo hadi leo haukupatikana jambo linalofanya lishindwe kujiendesha.
Aliongeza kuwa Serikali ilipoamua kutenganisha Shirika la Posta na Kampuni ya Simu (TTCL) mwaka 1994 baada ya kuvunjwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu, Serikali kwa mujibu wa sheria iliyounda Shirika la Posta iliazimia kutoa mtaji ili lijiendeshe vyema kibiashara.
“Hata hivyo kwa masikitiko makubwa toka mwaka huo wa 1994 hadi leo Shirika la Posta halijawezeshwa kimtaji na Serikali ambayo ndio mwenye mali,” alisema Makuke.
Aliongeza kuwa kipimo kizuri cha utendaji kazi hivi sasa ni uwezo wa mtaji na akaongeza kuwa iwapo kuna mtaji ni rahisi kuwatathmini viongozi katika ufanisi wao.
“Ombi letu kwa Serikali yetu tunaomba Shirika la Posta kuwezeshwa mtaji wa kujiendesha katika mwaka huu wa fedha,” alisema mwenyekiti huyo.
Alisema uwezeshaji wa Shirika la Posta kimtaji unaweza usiwe na fedha taslimu ili shirika lifikie malengo tarajiwa, ni lazima Serikali itoe maamuzi mazito na mwongozo kwa taasisi zote za Serikali na Wakala za Serikali kutumia huduma zinazotolewa na shirika hilo kwa ajili ya usafirishaji wa barua, vifurushi na vipeto.
Alisema kwa sasa inasikitisha kuona baadhi ya taasisi za umma zimekuwa zikitumia kampuni binafsi katika kusafirisha vifurushi, barua na vipeto jambo ambalo alisema Tewuta inaamini kuwa halifanyiki kwa maslahi ya Taifa, bali ni kwa maslahi binafsi.
No comments:
Post a Comment