Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, lengo la hatua hiyo ni kuzifanya shughuli hizo zitoe ajira zaidi kwa vijana.
Mahiza aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, alipofanya ziara iliyolenga kukagua shughuli za Mamlaka ya Bandari (TPA) Tanga.
Shughuli kuu inayofanywa kwenye bandari hizo 19 zisizo rasmi zaidi alisema ni ushushaji wa mizigo mbalimbali kutoka mjini Zanzibar, Mombasa na Brazil ambako bidhaa kama nguo na sukari hununuliwa kwa nusu ya bei iliyoko sokoni hapa nchini.
Alisema kutokana na changamoto ya uwepo wa bandari hizo bubu katika wilaya za Pangani, Muheza, Tanga na , uongozi wa mkoa umeamua kubuni mpango ambao utatumia tatizo hilo kama fursa ya kuongeza ajira kwa vijana na serikali kupata mapato.
“Hali ya ulinzi na usalama iko vizuri lakini changamoto iliyopo ni uwepo wa bandari bubu nyingi ambazo hutumika kukwepa kodi kutokana na wafanyabiashara kuingiza bidhaa mbalimbali ikiwemo sukari kutoka nchini Brazil, hatua ambayo inaathiri sana ushindani katika soko kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini,” alisema Mahiza.
Aliongeza: “Baada ya kuona bandari bubu hizi ni changamoto, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huu imeona kuzifunga halitakuwa suluhisho, badala yake imekuja na wazo ambalo tumeanza kulifanyia kazi.”
Akizungumzia sukari ya magendo inayoingizwa nchini kupitia bandari bubu ya Kigombe ambayo ilikamatwa mwezi uliopita, mkuu huyo alisema tayari wamekamilisha taarifa za uchunguzi na wahusika watachukuliwa hatua.
“Mheshimiwa Waziri, tunaunga mkono agizo la Rais wetu la kupiga marufuku uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi na kwa upande wetu kimkoa tayari unazo taarifa za vyombo vinavyohusika na biashara hiyo,” alisema.
Alisema mkoa umeshajua vyombo vinavyohusika kuingiza sukari ya magendo ni vya akina nani, wanaishi wapi na maeneo yote ikiwemo nyumba wanakohifadhia hiyo sukari kutoka Brazil.
“Changamoto tuliyonayo kwa sasa, tumebaini kwamba sukari hii inahusishwa na watu wazito wakiwemo viongozi wa kisiasa na kiserikali ambao wanazo kinga zao kisheria,” alisema.
Mkuu huyo alimweleza waziri kwamba pamoja na changamoto ya wasambazaji hao hivi sasa mkoa unaendelea kuelimisha wananchi katika wilaya zote zenye bandari bubu ili kuwawezesha wakazi kutumia haki na wajibu wao kisheria kuhusu tatizo hilo.
Waziri Ngonyani alisema dhana hiyo ya kushushia mizigo katika bandari bubu itakuwa na maana endapo tu uongozi wa mkoa utajiridhisha kwamba hapatakuwepo na namna yoyote ile ya ukwepaji wa kodi ya serikali.
No comments:
Post a Comment