Monday, 29 February 2016

Uzinduzi wa Albamu ya USIDANGANYIKE


 




































 Uwezo Alfayo mwamuziki wa nyimbo za injili Tanzania na Afrika Mashariki




 





































 Bw Uwezo Alfayo





 























 Muonekano wa nje wa Kasha la DVD ambayo inatarajiwa kuzinduliwa tar 10/04/2016




  
Mwimbaji  wa njimbo za injili Tanzania na Afrika mashariki  na aliyekuwa mwanafunzi  katika  chuo cha uandishi wa habari na utangazaji  Arusha  Ndg Uwezo Alfayo  anatarajia kuzindua albamu yake ya kwanza   ya video inayotambulika kwa jina la MSIDANGANYIKE

Albamu hiyo ya Usidanganyike imebeba  jumla ya nyimbo 10 na anatarajia kuzindua albamu hiyo mwanzoni mwa mwezi wan ne tar 10 mwaka huu katika la TAG Betheli Kijenge kwa Askofu Olsosy maarufu kwa jina la Sosy

Ambapo atasindikizwa na waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchini Tanzania  wakiongozwa na Joseph Nyuki,Kwaya ya  mama Jusi  kutoka Moshi,Kwaya ya Tumaini na waimbaji wengine wengi
Mwimbaji huyo alianza kazi yake ya kumsifu Mungu kwa  njia ya sifa mnamo mwaka 2011 akiwa chini ya Mchungaji Simon Moris ambaye anatoa huduma ya kiroho Longido

Pia aliwahi kuwa mwalimu wa shule ya secondary ya Mwasiku inayopatikana Igunga Mkoani Tabora

Lekule Laizer, Mwenyekiti wa CCM Arusha





CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, kimepata mwenyekiti ambaye ni Lekule Laizer atakayeongoza kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha, mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Shaaban Mdoe amechaguliwa kushika nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Arusha baada ya kuwashinda Semmy Kiondo na Veraikunda Urio kwenye uchaguzi uliofanyika juzi.
Uchaguzi wa kuwapata viongozi hao ulifanyika jijini hapa chini ya usimamizi wa mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Stephen Wassira. Laizer alikuwa akipambana na Emmanuel Makongoro na John Pallangyo kabla ya kupigiwa kura awamu ya kwanza na kubaki mawili; la kwake na Makongoro.
Idadi ya wajumbe ilikuwa 903 na kura zilizopigwa ni 861 huku tisa zikiharibika. Laizer alishinda kwa kupata kura 515 dhidi ya Makongora aliyepata kura 338. Kwa upande wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi, Mdoe alipata kura 36 dhidi ya Urio aliyepata kura 12.
Awali, akizungumza na wajumbe wa mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, Wassira alisema wanachama wakiwemo wenyeviti wa wilaya waliokisaliti watafukuzwa chama bila kujali vyeo au utajiri walionao.
Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Mkoa wa Arusha, Catherine Magige alimuomba Wassira kumpelekea Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete malalamiko akisema wana vidonda vinavyotokana na wanachama wenzao mkoani humo waliokisaliti chama.
Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Monduli, Namelock Sokoine alisema yeye ni mwanachama thabiti na jasiri ndiyo maana hakuzolewa na mafuriko ya kumfuata Edward Lowassa aliyehama CCM kwenda Chadema

Kuna mbinu mpya za kusafirisha mirungi




Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Mihayo Msikhela

POLISI mkoani Tanga imesema imegundua mbinu mpya ya usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi kwa kuziweka kwenye madumu tupu yaliyokuwa na mafuta.
Mbinu hiyo inadaiwa kutumiwa na baadhi ya wasafirishaji wa dawa hizo kuziingiza mkoani humo wakikwepa kukamatwa na askari kwenye vizuizi barabarani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Mihayo Msikhela aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kwamba wasafirishaji hao hujaza mirungi ndani ya madumu matupu ya ujazo wa lita 20 yaliyokuwa na mafuta ya kupikia na kisha kuyasafirisha katika magari mbalimbali ya mizigo.
Alisema wamebaini mbinu hiyo kutokana na jitihada za askari waliokuwa doria katika kizuizi cha polisi kilichopo eneo la Amboni kati ya saa 10 hadi 11 jioni baada ya kukamata lori namba T 342 CVY aina ya Nissan lililokuwa likisafirisha mchanga kwa ajili ya ujenzi kutoka kijiji cha Mpirani kwenda jijini Tanga.
“Jana jioni askari waliokuwa doria nje ya mji eneo la Mpirani lililopo kata ya Chongoleani walikamata watu saba waliokuwa wakisafirisha kilo 73 za mirungi kwa kutumia lori la mchanga kwa kuweka dawa hizo ndani ya madumu yaliyokuwa yametumika kuhifadhia mafuta ya kula na kisha kuyafunika na kifusi cha mchanga kilichokuwa ndani ya lori hilo”, alisema.
Aliongeza, “Baada ya kujaza mirungi madumu hayo waliyafukia ndani ya shehena ya mchanga uliokuwa unasafirishwa kwenda eneo la Kwanjeka jijini Tanga kuuzwa kwa mteja”, alisema.
Kamanda Mihayo aliwataja watuhumiwa wanane waliokuwa wakisafirisha mirungi hiyo ambao wote ni wakazi wa mkoani hapa, akiwemo dereva wa lori.
Alisema wote watafikishwa mahakamani.

Rais awasili Arusha tayari kwa mkutano EAC

Rais John Magufuli akisalimiana na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliyekuwa mmoja wa viongozi na wananchi waliojitokeza kwa wingi kumpokea alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kuongoza mkutano wa 17 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha. (Picha na Ikulu).

RAIS John Magufuli amewasili mkoani Arusha ambako pamoja na mambo mengine ataongoza Mkutano wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika keshokutwa mjini hapa.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Rais Magufuli alilakiwa na viongozi wa serikali, vyama vya siasa pamoja na vikundi vya burudani za ngoma kabla ya kuelekea Arusha Mjini.
Rais Magufuli ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Kabla ya kuongoza kikao hicho, Rais Magufuli anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alhamisi wiki hii, Magufuli na Rais wa Kenya, wataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha - Holili - Taveta - Voi inayounganisha Tanzania na Kenya.
Barabara hiyo ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayotekelezwa na nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Sunday, 28 February 2016

Yanga yang’ara Afrika





Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la pili lililofungwa na Thaban Kamusoko (wa pili kulia) kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius Uwanja wa Taifa, Dar es Salaa jana. Wengine kutoka kushoto ni Vicent Bossou, Deus Kaseke, Simon Msuva na Juma Abdul. (Picha na Rahel Pallangyo).
Yanga imeleta heshima kwa Watanzania baada ya jana kuifunga Cercle de Joachim ya Mauritius mabao 2-0 katika mchezo wa maruadiano Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kutokana na matokeo hayo Yanga imefuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 3-0, baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Mauritius wiki mbili zilizopita Yanga kushinda bao 1-0.
Yanga itakumbana na mshindi wa mchezo kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland.
Ilikuwa furaha kwa mashabiki wa Yanga walioingia jana kifua mbele ikiwa ni wiki moja baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya watani wao Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hata hivyo Yanga licha ya ushindi huo, itabidi ijilaumu kutokana na kukosa nafasi nyingi za wazi, ambazo zingewawezesha kupata ushindi mnono.
Lakini washambuliaji wake wakiongozwa na Amis Tambwe, Simon Msuva, Malimi Busungu na Paul Nonga kwa nyakati tofauti walishindwa kulenga lango la wapinzani wao.
Washambuliaji hao kila walipokaribia lango la Yanga, ama walipiga michomo dhaifu iliyodakwa na kipa au walipiga nje ya lango.
Yanga ilianza kupata bao la mapema dakika ya tatu mfugaji akiwa Amiss Tambwe kutokana na krosi ya Simon Msuva.
Bao hilo liliwapa matumaini mashabiki wa Yanga kuona ushindi mnono, lakini kadri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo matumaini hayo yalipokuwa yakififia.
Wageni walijitahidi kupanga mashambulizi dakika za mwanzo kipindi cha pili, lakini walijikuta wakipachikwa bao la pili dakika ya 56 mfungaji akiwa kiungo Thabani Kamusoko kwa shuti lilitokana na mpira wa adhabu wa Juma Abdul.
Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondani, Vincent Bossou, Mbuyu Twite/Pato Ngonyani, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Malimi Busungu/Paul Nonga na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya.
Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la pili lililofungwa na Thaban

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amuunga mkono Jecha



MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju amemuunga mkono Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kwa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na kusema hatua hiyo ni halali kutokana na sababu zilizotajwa.
“Ukichukua kasoro zote na hii ya mgombea kujitangaza mshindi... ni tatizo kubwa, lazima mtaingia kwenye matatizo iwapo huyu kajitangazia ushindi halafu matokeo yamtangaze mshindi tofauti na huyo,” alisema Masaju.
Akizungumza kwenye kipindi cha Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano, kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), juzi usiku, Mwanasheria huyo alisema ZEC iko huru kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na uamuzi uliofanywa na Mwenyekiti wa Tume hiyo ni kitendo halali.
Masaju alisema kasoro zote zikichunguzwa, ikiwemo hiyo ya mgombea kujitangazia ushindi, kulikuwa na kila sababu ya kufuta matokeo hayo ili uchaguzi urudiwe.
Alisema iwapo dosari hizo, zingeachwa bila kufanyiwa kazi, hata wagombea wasio na sifa ya kushinda katika uchaguzi huo, wangesema na wao ni washindi hivyo kungetokea machafuko ambayo yangeweza kuleta matatizo makubwa zaidi.
Ila kwa hatua iliyochukuliwa na ZEC ni jambo sahihi la kurudisha amani na kupanga tarehe nyingine ya kurudia uchaguzi huo, ili kasoro hizo zirekebishwe na mshindi apatikane kwa haki na kuepuka machafuko.
Masaju alisema awali Rais John Magufuli wakati akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe, alisema atashirikiana na Rais wa Zanzibar kumaliza suala la uchaguzi, ila hakusema ataingilia uhuru wa Tume.
“Rais alipohutubia Bunge kwa mara ya kwanza aliahidi kushirikiana na Rais wa Zanzibar kumaliza suala la uchaguzi, ila hakusema ataingilia uhuru wa Tume na ndicho alichofanya, Zanzibar ina amani,” alisema Masaju.

Sinema ujambazi wa kivita jijini Dar



UJAMBAZI wa kutumia vifaa vya kivita umeibuka jijini Dar es Salaam, ukiwemo uliofanyika katika uporaji wa Benki ya Access juzi, ambako majambazi walitumia bunduki za kivita aina ya SMG na mabomu ya kurusha kwa mkono.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema mbali na uvamizi huo, pia Polisi imebaini na kukamata askari bandia, waliokuwa na sare rasmi za Jeshi la Polisi zenye vyeo na redio call, zenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya askari Polisi.
Akizungumzia matukio hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alisema atakutana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, ili Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi, waanzishe msako wa pamoja dhidi ya wahalifu hao.
Uvamizi, mauaji Mbagala
Akisimulia ujambazi uliofanyika katika Benki ya Access Tawi la Mbagala, Kamanda Sirro alisema majambazi hao walikuwa 12, wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki sita na walifika kwenye benki hiyo saa 8:30 mchana.
Baada ya kufika, moja kwa moja waliingia kwenye chumba cha askari wanaolinda benki na kumpiga risasi kichwani askari mwenye namba H7739 Konstebo Harid na kufa papo hapo.
Mbali na mauaji hayo, Kamanda Sirro alisema walimshambulia askari mwingine, Konstebo Shaban miguuni na kupora silaha zao na kuingia nazo ndani ya benki, ambako walimshambulia mlinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi na raia wengine wawili na kufa papo hapo, huku wengine watano wakijeruhiwa.
Baada ya hapo kwa mujibu wa Kamanda Sirro, majambazi hao walikimbilia chumba kinachohifadhi fedha nyingi (strong room) na kukipiga risasi katika jitihada ya kutaka kuingia ndani, lakini hawakuweza kuvunja.
Kutokana na ugumu wa kuvunja chumba hicho, Kamanda Sirro alisema haraka haraka wakahamia katika kaunta za watoa fedha na kupora fedha zilizokuwepo kati ya Sh milioni 20 mpaka Sh milioni 30 na kuondoka na silaha za polisi aina ya SMG mbili na ile yao moja pamoja na pikipiki zao.
Polisi waua watatu
Kamanda Sirro alisema taarifa zilisambazwa katika vikosi vya ulinzi, ambavyo vilijiimarisha.
Alitaja Kikosi cha Mbwa na Farasi eneo la Mkuranga, ambao walijiandaa na majambazi hao walipofika kijiji cha Chui wilayani Mkuranga mkoani Pwani, walipambana na polisi na askari wakafanikiwa kuua majambazi watatu.
Mbali na kuua watatu, silaha tatu zilikamatwa ambazo ndio zile SMG mbili za Polisi, walizochukua pamoja na ile yao moja, lakini wakakutwa pia na mabomu matatu ya kutupa kwa mkono yaliyotengenezwa Urusi.
“Hawa majambazi walikuwa wamejiandaa, kwa maana walikuwa na mabomu ya kutupwa kwa mkono matatu aina ya RGD 01 ambayo ni mbinu ya kujilinda wanaposhambulia,” alisema Kamanda Sirro.
Tisa watoroka
Pamoja na kujiimarisha kwa polisi, majambazi tisa walikimbia wakaacha pikipiki zote sita za aina tofauti, ambazo ni Haojue mbili zenye namba MC 560 AED na MC 207 BAN, San LG yenye namba MC 784 BDJ, Boxer yenye namba MC 248 AXE na King Lion mbili zenye namba MC 653 BDQ na MC 853 BDR.
Kamanda Siro alisema baada ya hapo, waliendelea kuwakimbiza majambazi hao hadi wakatokomea katika Msitu wa Kongowe, ambako juhudi za kuwatafuta zilianza mara moja.
“Nawahakikishia wananchi mtandao wote wa ujambazi kwenye mabenki na maeneo mengine, tutausafisha wote kwa maana hawa wanafanya uhalifu maeneo ya Dar es Salaam na Pwani na wana ndugu zao, tutawakamata wote,” alisisitiza Kamanda Sirro.
Alisema hawawezi kuona Watanzania wakiumia na kufa kwa tamaa za wachache, wenye kupenda utajiri wa haraka.
JWTZ kazini
Akizungumza kuhusu ujambazi huo, Waziri Kitwanga alisema Polisi inajipanga upya na atazungumza na Waziri mwenzake, Dk Mwinyi kuangalia jinsi ya majeshi hayo mawili, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), watakavyofanya kazi pamoja ya msako katika misitu yote inayozunguka mikoa ya Pwani, kuanzia Bagamoyo hadi Kisarawe.
Alionya kama kuna kambi za uhalifu ndani ya misitu hiyo, zitasambaratishwa na kuomba raia wema watoe taarifa za uhalifu.
“Tutafanya operesheni kubwa na tutaifanya haraka, tunaomba wananchi watoe ushirikiano hasa waendesha bodaboda kwa maana zinatumika sana kwenye matukio haya. Mtandao wa majambazi ufahamu kwamba vyombo vya usalama havijalala, tutawamaliza wote, tutatumia nguvu zetu zote kuwamaliza na tutafanikiwa,” alisisitiza Kitwanga.
Kuhusu waendesha bodaboda, Kitwanga alisema ukaguzi wa kina unafanywa na kuwataka waendesha bodaboda hao wanaposimamishwa, wakubali na kutoa ushirikiano na wasione kama wanabughudhiwa, bali ni kuwakagua kwa sababu wahalifu hutumia vyombo hivyo zaidi kufanya matukio mabaya.
Polisi feki
Katika tukio jingine, Kamanda Sirro alisema polisi feki wanne wamekamatwa na wanashikilia kwa mahojiano, ili kubaini mtandao huo ambao unatumia sare za Polisi, redio za upepo na pingu kufanya matukio ya uhalifu.
Alisema walipata taarifa kutoka kwa raia wema ya kuwepo kwa mtandao wa askari bandia, ambao hutumia sare za jeshi hilo kufanya matukio ya uhalifu, ndipo walipowakamata hao wanne. Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, polisi feki watatu walikamatwa Februari 24, asubuhi saa mbili eneo la Upanga karibu na Daraja la Selander.
Alisema watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, walikiri kufanya matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja anayeishi Kinyerezi. Kamanda Siro alisema Polisi walimfuata mtuhumiwa huyo nyumbani kwake Kinyerezi na walipofanya upekuzi, walimkuta na sare halisi ya Polisi, redio ya upepo na pingu.
Kamanda Sirro alisema baada ya uchunguzi, imebainika kwamba watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia sare na vifaa hivyo vya Polisi, kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi kwa kujiaminisha kuwa wao ni askari Polisi.
Alisema watuhumiwa hao wamekiri kufanya matukio mbalimbali, ikiwemo kuweka vizuizi katika barabara za mikoani na kufanya uporaji.
“Watuhumiwa hao wote wanahojiwa ili waeleze jinsi walivyopata sare na vifaa hivyo ya Polisi, wamekiri kufanya uhalifu maeneo mbalimbali, lakini wakati mwingine tunashindwa kukamata wahalifu kwa sababu redio call wanayotumia zinaingiliana na zetu, hivyo wanakuwa wamepata taarifa,” alisema Kamanda Sirro.
Katika tukio lingine, Februari 18 mwaka huu, watuhumiwa watatu wa ujambazi, walikamatwa eneo la Kiwalani Kwa Mkude jijini Dar es Salaam wakiwa na bastola moja.

Ufisadi wa vitabu waathiri darasa la kwanza



Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Teknolojia, Sayansi na Ufundi, Maimuna Tarishi akitoa tamko la Serikali la kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) baada ya kushindwa kutekeleza maagizo ya kusitisha uchapaji wa vitabu vya kiada kwa darasa la kwanza ambavyo vilikuwa na kasoro. Mwingine ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Leonard Akwilapo. (Picha na Fadhili Akida).

UFISADI uliofanyika katika uchapaji wa vitabu 2,807,600, vilivyo tayari kutumika kwa ajili ya darasa la kwanza nchi nzima, umesababisha wanafunzi hao, ambao mwaka huu udahili wao umeweka historia kwa idadi kubwa kuwahi kudahiliwa, kulazimika kutumia vitabu vya zamani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna Tarishi (pichani), alisema hayo jana alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam. Alifafanua kwamba kasoro kubwa, zilizobainika katika vitabu hivyo, ambavyo vilishafika katika ghala la Serikali, zimesababisha Serikali izuie visisambazwe.
Kwa mujibu wa Tarishi, vitabu hivyo vya ‘Najifunza Kusoma Kitabu cha Kwanza’ na ‘Najifunza Kusoma Kitabu cha Pili’, vimechapwa na kampuni ya Yukos Enterprises, ambayo ni moja ya kampuni tatu zilizoshinda zabuni ya kazi hiyo iliyotangazwa Aprili mwaka jana.
Lakini, alisema kasoro hizo zimesababisha Serikali kuagiza viondolewe katika ghala lake na udhibiti ufanyike visisambazwe mashuleni.
Upungufu
Kasoro zilizokutwa ni muingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa, picha moja kuwa na rangi tofauti, ukataji usiozingatia vipimo, baadhi ya vitabu kufungwa kwa pini moja katikati badala ya mbili, huku vingine vikikosa pini kabisa na vingine vikifungwa ubavuni.
Kasoro nyingine ni vingine vimekutwa vimechakaa kabla ya matumizi, hasa kitabu cha ‘Najifunza Kusoma Darasa la Kwanza Kitabu cha Pili’; vingine vikiwa na mpangilio mbaya wa kurasa, ufifiaji wa maandishi huku picha katika baadhi ya vitabu na maandishi, vikishindwa kuonekana kabisa.
Kasoro nyingine kwa mujibu wa Tarishi ni namba za kurasa kutoonekana kabisa, baadhi ya kurasa kujirudiarudia, baadhi ya kurasa kutotenganishwa, maandishi ya baadhi ya vitabu kugeuzwa mwelekeo, majalada kuwa zaidi ya moja na baadhi ya vitabu kukutwa vimedurufiwa (photocopy).
Katibu Mkuu huyo alisema kasoro hizo, zilibainika baada ya ufuatiliaji kufanywa na Wizara katika bohari iliyokuwa ikipokea vitabu hivyo.
“Kutokana na kasoro hizo, ni dhahiri mchapaji Yukos Enterprises Ltd hakuzingatia vigezo vilivyowekwa na kwa kufanya hivyo amekiuka makubaliano yaliyo katika mkataba alioingia na Taasisi ya Elimu Tanzania,” alisema Tarishi.
Athari zake
Kutokana na hali hiyo, Tarishi alisema wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka huu watapungukiwa vitabu vya kujifunza kusoma, kwa kuwa haviwezi kutumika. Hivyo aliagiza wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka huu, watumie vitabu vya zamani na walimu watatumia ‘Kitabu cha Kiongozi cha Mwalimu’ ambacho ni kipya.
Kuhusu gharama iliyotumika, Tarishi alisema ni zaidi ya Sh bilioni mbili, lakini alibainisha kuwa mchapishaji alikuwa amelipwa asilimia 20 tu kwa kutumia dhamana ya benki.
Majipu yatumbuliwa
Kasoro hizo zimemlazimu Katibu Mkuu huyo kuagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), kuwasimamisha kazi vigogo wa taasisi hiyo, akiwemo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Vifaa vya Kielimu, Peter Bandio, Mwanasheria, Pili Magongo na Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Jackson Mwaigonela.
Hatua hiyo imetakiwa kufuatia uchunguzi katika taasisi hiyo, kuhusu vipi wameshindwa kusimamia Sheria ya Manunuzi na kazi ya uchapaji wa vitabu.

Saturday, 27 February 2016

Ulinzi waimarishwa Kili Marathon


ZAIDI ya askari 200 kusimamia mbio za 14 za Kilimanjaro Marathoni zitakazofanyika kesho mjini Moshi, imebainishwa.


Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAA), Amini Kimaro alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili kuhusu maandalizi ya mwisho kuhusu mbio hizo.
Kimaro alisema mbali na askari polisi ambao watalinda usalama katika maeneo mbalimbali zitakapofanyikia mbio hizo, pia kutakuwa na wasimamizi wengi ili kuhakikisha washiriki hawakatishi njia.

Kumekuwa na malalamiko mengi kuwa baadhi ya wanariadha wanaoshiriki mbio hizo kukatisha njia ili kupata ushindi. Alisema mwaka huu kila baada ya kilomita tano mbali na kuwa na vituo vya maji, pia kutakuwa na waangalizi ambao watakuwa wakirekodi namba za wakimbiaji ili wasikatishe njia.
Kimaro alisema kuwa pia kutakuwa na vifaa maalumu vya kielektroniki kufuatilia mwenendo mzima wa washiriki na kuhakikisha hakuna anayejaribu kukatisha njia.

Alisema kuwa kutakuwa pia na magari ya kuongoza mbio hizo pamoja na magari ya wagonjwa yatakayokuwa nyuma ya wakimbiaji wa mbio mbalimbali.

Alisema mbio za kilomita 42 zitaanza saa 6:30 huku zile za nusu marathoni za Tigo zitaanza saa 12:45 asubuhi wakati za kilomita 10 za walemavu zitaanza kutimua vumbi saa 1:00 asubuhi. Alisema mbio za kujifurahisha za kilomita tano zenyewe zinataraja kuanza saa 1:30 asubuhi.

Cheka mtihani mgumu leo



NANI kugeuka kitoweo kati ya Francis Cheka na Geard Ajetovic?
Leo litapigwa pambano la kimataifa la ubingwa wa mabara kwenye viwanja va Leaders, Dar es Salaam huku mabondia wote wawili wakitambiana kumalizana.
Mabondia hao wanapigania uzito wa kilo 72 ubingwa wa mabara, ikiwa ni mara ya pili kukutana baada ya mwaka 2008 kukutana kule Manchester nchini Uingereza ambapo Cheka alipigwa kwa pointi.
Cheka alisema jana kuwa hatawaangusha Watanzania kwani amejipanga kumgeuza Ajetovic kitoweo.
“Naahidi kwamba mkanda huu wa dunia utabaki nyumbani, sitawaangusha Watanzania, watu waje kwa wingi kushuhudia watajua nani kuwa bingwa,” alisema.
Bondia huyo wa Tanzania alizungumza kwa maneno ya kimakonde kutamba kuwa kilichoumbwa na Mungu sio haramu kuliwa, hivyo, ni halali yake kummaliza bondia huyo wa Uingereza mapema na kuwa kitoweo chake.
Kwa upande wa Ajetovic alisema atammaliza Cheka kwa KnockOut (KO) raundi ya nne tu na kuuchukua mkanda huo.
Alisema amejipanga kushinda hivyo hana wasiwasi huku akimwita Cheka kuwa ni babu hana lolote. Pambano hilo la kimataifa litasindikizwa na burudani kutoka bendi ya Twanga Pepeta.

Infantino Rais mpya Fifa



KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-Uefa, Gianni Infantino amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Soka duniani-Fifa.
Infantino alishinda awamu ya pilii ya uchaguzi huo uliofanyika Uswisi kwa kura 88 kati ya kura 207 akifuatiwa na Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa wa Bahrain aliyepata 85.
Mwanafalme wa Jordan Ali Bin Hussein alipata kura 27 na mgombea kutoka Ufaransa Jerome Champagne alipata kura saba.
Infantino mwenye umri wa miaka 45 anashika nafasi hiyo kumrithi Sepp Blatter aliyesimamishwa kushiriki shughuli zozote za soka kwa miaka minane adhabu ambayo ilipunguzwa kuwa miaka sita pamoja na Rais wa zamani wa Uefa Michel Platini kwa tuhuma za rushwa.
"Ndugu zangu, siwezi kuelezea hasia zangu kwa wakati huu," Infantino alisema wakati akizungumza baada ya kuchaguliwa. "Tutarejesha hadhi na heshima ya Fifa. Watu watatupongeza, watawapongeza ninyi kwa mabadiliko tutakayofanya."

Yanga yatangaza raha


KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm

WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, leo wataikabili Cercle de Joachim ya Mauritius ukiwa ni mchezo wa marudiano hatua ya awali.
Katika mchezo wa kwanza ugenini Uwanja wa George V, Yanga ilishinda bao 1-0, matokeo ambayo yanawapa Yanga kazi nyepesi leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutinga hatua inayofuata kwani inahitaji angalau sare.
Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm, amejitapa kushinda mchezo huo baada ya maandalizi mazuri waliyofanya kwa wiki mbili tangu warejee nchini.
Pluijm ambaye katika mchezo huo atawakosa nyota watatu wakiwemo wawili wa kimataifa, Haruna Niyonzima na mfungaji wa bao pekee lililowapa ushindi ugenini Donald Ngoma, alisema pamoja na kuhitaji sare, lakini lazima washinde.
“Tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda mchezo wa kesho (leo), kwa sababu tumefanya maandalizi ya kutosha na tunacheza nyumbani mbele ya mashabiki wetu hatutapenda kuwaangusha na kizuri zaidi tunawajua vizuri wapinzani wetu,”alisema Pluijm.
Pluijm alisema pamoja na kuwakosa nyota hao, lakini ana imani kubwa na wachezaji waliopo ambao ana hakika watacheza kwa kiwango cha juu na kuwapa ushindi. Wapinzania wa Yanga, Cercle de Joachim, tayari wametua Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo huo huku wakionekana wamejipanga kuhakikisha wanalipa kisasi.
Kocha wa timu hiyo, Abdel ben Kacem, amesema amewajua vizuri Yanga na kwa maandalizi waliyoyafanya anaamini atafanikiwa kulipa kisasi. Katika hatua nyingine, kocha wa Simba, Jackson Mayanja, ameitabiria ushindi Yanga katika pambano la leo kwani wapinzani wao ni timu ambayo haina jina kubwa katika soka.
“Sitaki kuizungumzia sana Yanga, lakini nawapa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, kwa sababu wana timu nzuri na tayari wana akiba ya bao kufuatia ushindi walioupata ugenini, lakini hata timu wanayocheza nayo ni dhaifu,” alisema Mayanja.

Mawaziri ‘waliombip’ Magufuli hadharani

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

MAWAZIRI watano wamewekwa hadharani kuwa ndio hawakujaza Tamko la Rasilimali na Madeni na Hati ya Ahadi ya Uadilifu na kurejesha fomu hizo katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana asubuhi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Rais John Magufuli, aliagiza mawaziri hao watekeleze wajibu huo kabla ya saa 12.00 jioni, vinginevyo watakuwa wamejiondoa wenyewe katika nafasi zao.
“Rais ameelekeza mawaziri popote walipo warudi na kutekeleza hilo na ofisi yangu itasimamia kwa karibu kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni na Hati ya Ahadi ya Uadilifu. “Wafanye hivyo na kuzirejesha kabla saa 12 jioni na Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili, atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Majaliwa alisema Rais ameelekeza mawaziri hao watajwe ili popote walipo wajue na kurejea kuzijaza fomu hizo.
Kutokana na maelekezo hayo, Majaliwa aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, ambao hawajarudisha fomu zote mbili za Tamko la Rasilimali na Madeni na Hati ya Ahadi ya Uadilifu.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga ambaye alikuwa hajarejesha Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi wa umma na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ambaye alikuwa hajarudisha Tamko la Rasilimali na Madeni.
Waziri Mkuu alisema Naibu Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira), Luhaga Mpina, yeye alikuwa hajarejesha fomu zote mbili za Tamko la Rasilimali na Madeni na Hati ya Ahadi ya Uadilifu.
Aliweka msisitizao kuwa kiongozi yeyote wa umma, anatakiwa kujaza fomu ya kutamka mali na madeni kwa viongozi wa umma na kuhaidi uadilifu uliotukuka na sheria hiyo itaendelea kufanyiwa kazi kwa wote wanoendelea kuteuliwa.
Akizungumzia suala la mawaziri waliokuwa safari ambao pengine wangeshindwa kuwasilisha fomu hizo, Majaliwa alisema cha muhimu agizo limetolewa na sababu nyingine zitaangaliwa kama zina msingi.
Alisema kama mawaziri hao wako nje ya nchi, ni lazima Rais anajua kwani ndiye anayetoa kibali na ikiwa wako mikoani ambako hawataweza kufika mpaka jana jioni, Waziri Mkuu anafahamu hivyo wataangalia sababu hizo.
Waziri Mkuu amesema wakati akifungua mafunzo ya mawaziri na naibu mawaziri kuhusu Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu yaliyofanyika Ikulu juzi, alikabidhiwa majina ya mawaziri hao.
Akifafanua Majaliwa alisema kila kiongozi anawajibika kutoa tamko la mali na madeni ndani ya siku 30 baada ya kuteuliwa, mwisho wa kutumia wadhifa husika na kila mwisho wa mwaka.
Alisema mawaziri walikabidhiwa fomu hizo walipoteuliwa na viongozi wengine wameendelea kujazafomu hizo na kurudisha kwa Kamishna.
Akizungumza juzi katika mafunzo hayo, Kamishna wa Maadili Jaji mstaafu Salome Kaganda, alisema ofisi yake ilikuwa imepokea fomu za matamko ya mali kutoka kwa baadhi ya mawaziri na baadhi yao walikuwa hawajajaza fomu hizo wala za ahadi ya uadilifu.
Alisema Sheria ya Maadili inamtaka kila kiongozi, kuwajibika kuwasilisha tamko la mali kwa sekretarieti hiyo na jukumu la chombo hicho cha kusimamia maadili ya viongozi, ni kupokea fomu za tamko la kiongozi wa umma za rasilimali, maslahi na madeni.
Jukumu linguine alitaja kuwa ni kupokea, kuchambua na kuchunguza malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukiukwaji wa maadili unaodaiwa kufanywa na viongozi wa umma na kuandaa na kutunza daftari la rasilimali, maslahi na madeni ya viongozi hao.
Alisema sekretarieti hiyo ina wajibu wa kuratibu vikao vya Baraza la Maadili kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma na kuwasilisha kwa Rais taarifa hizo za uchunguzi.
Kwa mujibu wa jaji Kaganda, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, inatamka maadili yanayotakiwa kuzingatiwa na kila kiongozi kuwa ni uadilifu, haki na uwajibikaji ambazo ni sifa muhimu za kiongozi bora.
Jaji Kaganda alisema kwa kuzingatia misingi na miongozo hiyo, katika sheria hiyo mawaziri na wakuu wa mikoa wamewekewa kifungu maalumu kinachobainisha maadili wanayopaswa kuyatekeleza.

Ajali yaua wanne


WATU wanne wamekufa akiwamo daktari wa wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro, Albion Kasasa huku abiria wanane wakijeruhiwa kwa kukatika viungo mbalimbali vya miili yao baada ya basi dogo na gari kugongana katika barabara kuu ya kutoka Shinyanga maeneo ya Maganzo kwenda jijini Mwanza.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 10:30 jioni katika Kijiji cha Buganika, kata ya Songwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo basi dogo lenye namba za usajili T260 DDY aina ya Fuso, mali ya kampuni ya Mashimba ikitokea Kahama kwenda Mwanza kugongana na gari T281 CLJ Honda Station Wagon.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Mika Nyange alisema gari hilo dogo lilikuwa likiendeshwa na daktari kutoka Ifakara, Kasasa ambaye alikufa papo hapo huku majeruhi wakikimbizwa katika hospitali ya rufani mkoani Shinyanga.
Kamanda Nyange alitaja watu wengine waliokufa kuwa ni Ismail Hassani na Subira Elius wote wakazi wa Kahama na Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, Pius Emmanuel wakati majeruhi wanane ni Ramadhani Athumani, Amina Ally, Mwamvua Deo na Anastazia John.
Wengine ni Mrashi Abdalah, Juma Hamza, Ibada Lwegoshola na Ndalawa Mashigani. Kamanda Nyange alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa magari yote mawili .
Naye mmoja wa majeruhi hao Ramadhani Athumani alisema walikuwa wakitokea Kahama kwenda Mwanza na walipofika katika kijiji hicho cha Buganika, ghafla waliona gari dogo likiyumba.

Wanandoa wadaiwa kumuua mtoto wao


WATU wanne wamekufa akiwamo daktari wa wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro, Albion Kasasa huku abiria wanane wakijeruhiwa kwa kukatika viungo mbalimbali vya miili yao baada ya basi dogo na gari kugongana katika barabara kuu ya kutoka Shinyanga maeneo ya Maganzo kwenda jijini Mwanza.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 10:30 jioni katika Kijiji cha Buganika, kata ya Songwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo basi dogo lenye namba za usajili T260 DDY aina ya Fuso, mali ya kampuni ya Mashimba ikitokea Kahama kwenda Mwanza kugongana na gari T281 CLJ Honda Station Wagon.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Mika Nyange alisema gari hilo dogo lilikuwa likiendeshwa na daktari kutoka Ifakara, Kasasa ambaye alikufa papo hapo huku majeruhi wakikimbizwa katika hospitali ya rufani mkoani Shinyanga.
Kamanda Nyange alitaja watu wengine waliokufa kuwa ni Ismail Hassani na Subira Elius wote wakazi wa Kahama na Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, Pius Emmanuel wakati majeruhi wanane ni Ramadhani Athumani, Amina Ally, Mwamvua Deo na Anastazia John.
Wengine ni Mrashi Abdalah, Juma Hamza, Ibada Lwegoshola na Ndalawa Mashigani. Kamanda Nyange alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa magari yote mawili .
Naye mmoja wa majeruhi hao Ramadhani Athumani alisema walikuwa wakitokea Kahama kwenda Mwanza na walipofika katika kijiji hicho cha Buganika, ghafla waliona gari dogo likiyumba.

Friday, 26 February 2016

Wazazi Jijini Arusha watakiwa kupiga vita ukeketaji na ndoa za utotoni

Afisa  ustawi wa jamii Bw. Shija Numbu





Wazazi wamehaswa kuwalea watoto wao pindi wanapokuwa wadogo hadi wanapofikia umri wa miaka 18 na kuwapa huduma za msingi ambazo mtoto anazihitaji

Hayo yamesemwa na Afisa Ustawi wa Jamii Bw. Shija Numbu wakati akizungumza na mmiliki wa blog hii na kulezea kwa undani zaidi kuhusu majukumu ya mzazi kwa mtoto kwa mujibu wa sheria za haki za  watoto ya mwaka 2009

Amesema kwamba sheria hii inawataka wazazi kuwapa watoto elimu,malezi mazuri  bila kusahau afya  bora na kuhakikisha mtoto anakuwa katika muonekano mzuri

Mbali na hayo pia amesema kwamba ni kosa la jinai kwa mzazi kumuozesha mtoto wa kike aliyechini ya umri wa miaka 18 kwani atasababisha mtoto huyo kukosa haki ya kupata elimu  pia kusababisha kupata madhara kwa kubeba  mimba za utotoni

“Mtoto akiolewa chini ya umri wa miaka 18 kawaida viungo vyake  vya uzazi vinakuwa bado havijakaza hivyo akibeba mimba nirahisi sana kupata saratani ya kizazi “Alisema Bw. Shija

Hata hivyo amesema kuwa wazazi ndiyo ngazi ya kwanza  katika kupinga ndoa za utotoni pindi wanapoona watoto wao wanakwenda ndivyo sivyo ili waweze kuwasaidia kutimiza ndoto zao
Vilevile Bw. Numbu amezungumzia suala zima la ukeketaji kwa watoto na kusema kuwa dhana hiyo bado inaendelea katika mkoa wa Arusha  na kwa sasa wanatumia njia mbadala katika kutizimiza adha hiyo ya ukeketaji kwa watoto

“Kwa sasa wanawakeketa watoto wakiwa wachanga hivyo mtu si rahisi kujua  kwa sababu wanaogopa kutumia njia ya zamani  kwa kuwa watajulikana  hivyo bado tunaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha tunatokomeza dhana hii katika jamii” Alisema Numbu

Amesema kuwa hawajawahi kupokea kesi ya ukeketaji kwa wanawake  katika ofisi zao kwa sababu jamii inogopa  kwa kuhofia kuchukuliwa hatua za kisheria lakini mwaka 2012 walipokea kesi moja  ya ndoa za utotoni  na hadi sasa hivi hakuna kesi yeyote waliyowahi kupokea kuhusana na ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji



Thursday, 25 February 2016

Kila aaminiye Mungu humlinda

Ndani ya yesu kuna raha

ALBINO HAWANA HATIA tazama wimbo huu ili uweze kujifunza mengi na kuelimisha jamii

Wimbo huu unahusu Mauji ya Albino,vikongongwe ulioimbwa na Mr& Mrs Elihuruma Chao kwa lengo la kuhamasisha jamii kuepukana na mawazo hasi ya kwamba watatajirika kwa kuwaua watu wenye ulemavu wa ngozi

Chuo Kikuu St. Joseph wagoma



Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya
 
WANAFUNZI 1,548 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph tawi la Arusha, wamegoma kuingia darasani kwa siku tatu na kukodi mabasi matatu kwenda Dar es Salaam kumwona Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Lengo la safari yao hiyo ya Dar ni kujua hatma yao, baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kufungia chuo hicho tawi la Songea.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, alibainisha kuwa hatma ya chuo hicho, itatolewa rasmi kesho baada ya tume hiyo kupitia mapendekezo ya tume ya wataalamu iliyoundwa mapema kwa ajili ya ukaguzi wa chuo hicho, tawi la Arusha.

Kulikuwa na vurugu miongoni mwa wanafunzi juzi jioni, hali iliyofanya uongozi kufikia uamuzi wa kufunga chuo hicho kwa muda usiojulikana. Wakizungumza jana kabla ya kuanza safari kwenda Dar es Salaam kumwona Waziri Ndalichako, wanafunzi hao walisema mmiliki wa St. Joseph ni mmoja, hivyo kama tawi la Songea lina shida ni wazi matawi yote nchini yana shida.

Waliomba serikali kutoa ufafanuzi, kabla ya kuendelea kupoteza fedha za umma walizopatiwa kama mikopo.

“Pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu kutoa waraka kwenye mtandao kuwa kufungwa kwa chuo cha Songea, hakuhusiani na matawi ya chuo hicho, lakini sisi hatuna hakika tunataka watu hakikishie kama tupo salama,” alisema mwanafunzi Joel Lameck.

Aliendelea kusema, “na tukimaliza masomo yetu, je, tutapata ajira serikalini, yasije yakatukuta ya Chuo cha St. John cha Dodoma ambao hawakupata ajira kwa sababu elimu waliyopata haikuwa na viwango.

Wanafunzi hao ambao wengi wao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walisema wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kuwa chuo hicho kina upungufu mwingi, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kufundishia.

Pia wanafunzi hao walihoji sababu za serikali, kutowaleta wanafunzi wa tawi la Songea iwapo tawi lao la Arusha lipo salama, badala yake wamepelekwa vyuo vingine, nje ya St Joseph.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Siles Balasingh, aliomba serikali kutoa majibu haraka kwa wanafunzi hao wanaosomea ualimu wa masomo ya Sayansi, waendelee na masomo yao, kwani wamepata wasiwasi baada ya kufungwa tawi la Songea, japo hawana shida na chuo.

Alisema wao kama chuo, wamejitahidi kubandika chuoni hapo tangazo la TCU kwamba tawi hilo halihusiki na matawi mengine, lakini wanafunzi hawaelewi, wamegoma kuingia darasani, pia wameharibu mali za chuo.

“Hawa wanafunzi leo siku tatu hawataki kuingia darasani na wamekodi mabasi matatu wanaelekea Dar es Salaam kumwona waziri, lakini wamewapiga baadhi ya wanafunzi wenzao kwa kuwakataza kufanya mitihani mpaka wapate uhakika wa masomo tunayowapatia kama tumekidhi vigezo vya mitaala ya elimu,” alisema
.
Alisema walimu wanasikitika kuona vurugu zinatokea kwa sababu hiyo, hivyo ikiwezekana wanamwomba waziri wa elimu afike chuoni hapo, kutoa ufafanuzi ili wanafunzi wao hao wapatao 1,518 waendelee na masomo yao.

Hatma ya chuo kujulikana Ijumaa
Akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dar es Salaam jana, Profesa Mgaya alisema mgogoro wa chuo hicho, ulianza muda mrefu tangu mwaka 2014, hali iliyosababisha tume hiyo kufanya ukaguzi chuoni hapo.

“Tume iliunda timu ya wakaguzi iliyoongozwa na maprofesa wa taaluma mbalimbali, waliokagua mfumo wa ufundishaji, mazingira ya ufundishaji na kuhoji wanafunzi chuoni hapo. Tayari timu hii imewasilisha ripoti yake kwa TCU,” alisisitiza.

Alisema leo tume hiyo inatarajia kukutana na timu hiyo na Kamati ya Ithibati majira ya saa 3 asubuhi, kuijadili ripoti ya ukaguzi wa chuo hicho na saa 9 mchana itaitisha mkutano wa dharura kujadili mapendekezo ya taarifa hiyo na kutoa maamuzi dhidi ya chuo hicho.

“Tutautangazia umma Ijumaa (kesho) majira ya saa nne asubuhi kuhusu hatma ya chuo hiki cha St Joseph tawi la Arusha.

Wednesday, 24 February 2016

Nchi yangu Tanzania



 




















 Muonekano wa mapango ya Amboni yanayopatiana mkoani Tanga






















 Vijana wakiwa wanatoka ndani ya mapango ya Amboni


 






































Mapango ya amboni ni moja ya vivutio vikubwa vya kitalii nchini kwani yamekuwa yakipokea wageni tofauti tofauti wa ndani na nje ya nchi
Mpango haya yanapatikana katika kijiji cha Kiyomoni  kata ya Amboni  mkoani Tanga na inasemekana mapango haya yalikuwepo tangu miaka milioni 100 na 50(100,500,000) iliyopita
Miamba hii ilitokea baada ya tetemeko la  ardhi  miaka hiyo na katika mapango hayo  kuna miamba  ya chokaa  ambapo miamba hii inasaidia katika menginea shughuli za kiwandani kwa ajili ya kutengenezea chokaa ambazo zinatumika katika ujenzi na mambo
Akizungumzia historia hiyo ya mapango ya Amboni Bw. Allan amesema kwamba eneo hili lina ukubwa wa kilomita za mraba zipatazo 234
“Pia ndani ya miamba hii kulishawahi kupotea mzungu ambaye alikataa kuongozwa na mwenyeji wa eneo hili alipoingia mapangoni hajatoka hadi leo hii tangu miaka 8 iliyopita mzungu huyo aliingia na mbwa wake cha ajabu mbwa tulimuona na mzungu huyo hakuonekana na inasemekana kwamba aliingia kwenye mashimo ambayo yanaelekea mlima Kilimanjaro na kupotelea huko”Alisema Allan