Mshambuliaji
wa timu ya soka ya Taifa Tanzania, ‘Taifa Stars’, Elias Maguli (kulia)
akichuana na David Odhiambo wa Kenya ‘Harambee Stars’ wakati wa mchezo
wa kirafiki wa Kimataifa baina ya timu hizo uliofanyika Uwanja wa Moi
Kasarani, Nairobi, Kenya juzi. Timu hizo zilifungana 1-1. (Na Mpigapicha
Wetu).
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imerejea nchini
kutoka Nairobi, Kenya, ambako mwishoni mwa wiki ilicheza na wenyeji wao,
timu ya taifa ya nchi hiyo `Harambee Stars’ na kutoka nao sare ya 1-1
katika mchezo mkali wa kirafiki kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi.
Lakini baada ya kurejea jana asubuhi, timu hiyo imekwenda moja kwa
moja kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri Jumamosi wiki hii kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku kocha mkuu, Charles Boniface
Mkwasa akiapa `Misri hawatatoka’.
“Najua Misri wanatufuatilia. Na hata Kenya kwa siku zote tatu
walikuwepo. Najua Misri wanahitaji hata sare ili wafuzu kwa fainali
hizi, lakini hawataipata Tanzania,” alisema Mkwasa kwa msisitizo. Stars
na Misri zinakutana katika mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya
kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka kesho huko Gabon.
Katika mchezo wa kwanza mwishoni mwa mwaka jana, Misri wakiwa
nyumbani walishinda 3-0. Mkwasa alisema jana kuwa, kwa jinsi msimamo
ulivyo kwa sasa, Misri wanaifuatilia Stars na walikuwepo Nairobi
kushuhudia mchezo wao ili wapate mbinu za kushinda kirahisi, lakini
akaapa hilo walisahau.
Alisema pamoja na kuifanyia ushushushu Stars, Misri haitakuwa na
jeuri ya kuifunga Tanzania jijini Dar es Salaam, akisema ana uhakika
vijana wake watajitahidi ili kupata matokeo mazuri baada ya Jumapili
kufanya vema dhidi ya Harambee Stars.
Wakati Misri wana pointi saba, Taifa Stars ina pointi moja katika
kundi lao la G, hivyo sare yoyote kwa Misri itawahakikishia kufuzu kwa
fainali, lakini ikifungwa itaweka hai matumaini ya Tanzania kucheza
fainali za Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980.
Hata hivyo, itawezekana endapo itashinda ugenini dhidi ya Nigeria katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
“Kama nilivyosema, Misri wanahitaji pointi moja. Lakini sisi
tunahitaji pointi tatu. Mchezo wa Kenya unatosha kuona mapungufu. Maana
ilikuwa mechi ngumu iliyojaa nyota wote wa Kenya ambao ni professionals,
lakini mimi nilikuwa na local based players na matokeo yamekuwa hayo.”
Mkwasa alisema ana taarifa namna ambavyo Misri wanaifuatilia Taifa
Stars hususani ukusanyaji wa video kwa ajili ya kuona aina ya soka la
Tanzania, ambapo alisisitiza kuwa kamwe hawatafanikiwa. Kwa mara ya
mwisho Tanzania ilifuzu kwa fainali hizo za Afrika mwaka 1980 wakati
Mkwasa akiwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi hicho.
Mkwasa alipongeza Shirikisho la Soka Kenya (FKF), kwa kuandaa mchezo
huo angalau kwa asilimia 70 kwa kushirikiana na Tanzania iliyojazia
gharama sambamba na vijana wake kwa kucheza kwa kujituma licha ya
kuwakosa nyota wake wa kulipwa.
Taifa Stars ilicheza mchezo huo bila ya nyota wake wa kimataifa,
Mbwana Samata anayeichezea timu ya Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu
wa TP Mazembe ya DRC.
Naye Mwinyi Kazimoto aliyekuwa nahodha wa Stars dhidi ya Kenya,
alisema mchezo dhidi ya Kenya umewapa picha halisi ya utayari wao
kuwavaa Misri na kwamba, wako tayari kwa hilo.
Katika mchezo huo, nahodha wa Kenya, Victor Wanyama anayeichezea
klabu ya Southampton ya Ligi Kuu ya England, alielezea kushangazwa na
ubora wa kikosi cha Stars kilichoonesha soka maridadi licha ya kutokuwa
na nyota wake wanaocheza soka ya kulipwa nje ya Tanzania.